Mauaji yapungua asilimia 34 Geita

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama mkoani hapa imesaidia kupunguza takwimu za matuko ya mauaji ya kikatili kwa zaidi ya asilimia 34.

Kamanda Jongo amesema hayo mjini Geita mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya ‘Ongea Nao’ inayolenga kuzuia, kutanzua na kupambana na uharifu kwa kutumia jamii.

Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2022 yaliripotiwa matuko ya mauaji 49 lakini kwa Januari hadi Oktoba 2023 yameripotiwa matukio ya mauaji 32 pekee.

“Lakini matukio ya kubaka mwaka jana (2022) yalikuwa 86 na mwaka huu (2023) tuna matukio 75, huku matukio ya kulawiti mwaka jana yalikuwa saba na mwaka huu ni matukio sita.

“Lakini matukio ya shambulio la kudhuru mwili, mwaka jana tulikuwa na matukio 26 na mwaka huu tuna matukio 21, lakini matukio ya mimba za mashuleni mwaka jana zilikuwa 27 na mwaka huu tuna 25.

“Pia mwaka jana kulikuwa na matukio 39 ya kutekeleza familia lakini mwaka huu tuna matukio 20 tu, kwa hiyo kwa takwimu hizi chache mnaona namna gani hizi kampeni zinaenda zikipunguza uharifu.”

Amesema kushuka kwa takwimu hizo kumeifanya Geita kushika nafasi ya tano kitaifa kwenye idadi kubwa ya matukio ya ukatili hali inayotoa taswira na mwelekeo mzuri kwa hatua zilizochukuliwa na mkoa.

Amesema kitaifa kampeni ya Ongea Nao ilianza rasmi Agosti 30, 2023 ambapo kwa Geita walianza kwa kutembelea na kutoa elimu ya haki na sheria kwa makundi tofauti ili kudhibiti uharifu, ukatili na mauaji.

“Nia na madhumuni ya jeshi la polisi mkoa wa Geita ni kuiondoa kabisa Geita kwenye ramani ya matukio yeyote ya uharifu na hii naamini itawezekana kwa sababu takwimu zinaenda zinashuka.”

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amelipongeza jeshi la polisi kwa kuja na kampeni ya Ongea Nao na kuwaagiza viongozi wote ikiwemo wakuu wa wilaya kutoa ushirikiano ili kampeni hiyo iwe na tija.

Ameelekeza usimamizi thabiti wa kampeni ya Ongea Nao kuwa endelevu kwani pia itaenda kuungana na kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili ili kuhakikisha matokeo chanya yanaendelea kuonekana zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button