Mavunde: Leseni za madini kwa vikundi, si mtu mmoja

SHINYANGA: WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amesema leseni za uchimbaji madini hazitatolewa kwa mmoja mmoja, bali vijana wanapaswa kuunda vikundi ili wapate leseni na kuwa wamiliki wa migodi wasiishie kutumikishwa.
Mavunde amezungumza hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika machimbo ya mgodi mdogo uliopo kwenye kijiji cha Msasa mkoa wa kimadini Mbogwe ambapo amewaeleza wachimbaji wadogo kuwa leseni ambazo haziendelezwi zitafutwa maana tayari umefanyika uchunguzi wa maeneo hayo.

Amesema hata wale wanaofanya utafiti wafanye ndani ya miezi mitatu na waeleze kilichomo mfano leseni iliyokuwepo hapa ya uwekezaji kutoka Kampuni ya Stamico wamenyanga’nywa na itagaiwa kwa wachimbaji wadogo.
“Ninyi wachimbaji wadogo katika pato la taifa mnaingiza Sh trilioni 1 kwa mwaka sawa na 40% na eneo walipo wachimbaji wadogo ni utafiti tosha wakujua kuna madini ndiyo maana tunataka mbadilike muwe wamiliki wa leseni,”amesema Mavunde.

Rais wa Wachimbaji Wadogo (FEMATA), John Bina amesema wachimbaji wadogo serikali imewapa heshima kubwa nakutambua mchango walionao hivyo hakuna budi kupewa leseni wachimbaji wadogo waliopo eneo hili la Msasa ila changamoto inayowakabili hakuna maji na nishati ya umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema serikali imetoa maelekezo ya tafsiri ya utu na kazi na kazi inayofanywa ni kubwa lakini changamoto ya eneo hili kukosa nishati ya umeme na maji kuna mpango unaofanyika ili msiendelee kutumia mafuta katika shughuli zao za utafutaji madini.

“Mazoea yaliyokuwepo ya muda mrefu tunataka tuyaondoe yakae kimaadili hivyo Waziri wa Madini leo nakwambia migogoro hapa hakuna, wala mmiliki mwenye leseni kumfukuza mchimbaji mdogo asiye na leseni,”amesema Shigela.
Baadhi ya wachimbaji wadogo, Lea Bakari na Alphonce Majiku wameomba kero walizonazo zitatuliwe ili waweze kunufaika ikiwemo kuongeza asilimia katika mgawanyo wa mawe wanayoyapata na kupunguza ushuru wa mfuko wa mawe.




