Vijana sekta ya madini wahimizwa kupiga kura

MWANZA: UMOJA wa vijana katika sekta ya madini (TYM) umewahimiza wachimbaji wote nchini kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, ili kupata haki yao kikatiba.
Kwa niaba ya uongozi wa umoja huo, Mwenyekiti TYM Mkoa wa Mwanza, Cuthbert Joseph, amesema leo Oktoba 27, 2025 kwamba kupiga kura kutawasaidia pia kupata viongozi wanaowataka kwa ajili ya kuendelea kufanya maboresho zaidi katika sekta hiyo.
“Sisi tuko tayari. Wakati umoja unaanzishwa tulikuwa wananchama 600,000, na mpaka waliosajiliwa ni milioni nne,” amesema.

Wakati huohuo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwaboreshea mazingira ya uchimbaji, ikiwa ni pamoja na kurahisisha mchakato wa upatikanaji leseni za uchimbaji na utafiti.
“Tumepatiwa pia mitambo miwili ya kuchorongea dhahabu yenye thamani ya Sh bilioni 36. Vijana takribani 2,000 wamepata leseni ya uchimbaji katika mgodi wa Nyamongo mkoani Mara,”amesema.
Kadhalika Rais amesaidia kupungua kwa gharama za vifaa vya kuchorongea dhahabu, ambazo kwa sasa ni Sh 200,000 kwa mita moja, amesema.
Katibu wa Umoja huo, Ashraph Omary, pia aliwahimiza vijana kujitokeza kupiga kura, ikizingatiwa mamlaka husika zimewahakikishia ulinzi na usalama.



