SERIKALI imewataka wananchi wa vijiji saba katika Wilaya ya Tarime Vijijini kufuata sheria za mipaka na kutoendeleza shughuli za aina yoyote zinazohusisha kilimo na kutolisha mifugo katika maeneo yaliyowekwa vigingi vya mipaka katika Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angela Kairuki, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kegonga baada ya kutembelea vigingi vya mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na maeneo ya wananchi.
Alisema ujio wa mawaziri watatu, ambao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula, Kairuki na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja ni kwa ajili ya kutekeleza agizo la Waziri Mkuu alilotoa bungeni hivi karibuni.
Lengo ni kupata ukweli wa malalamiko ya Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambapo alidai kuwa vigingi viliwekwa bila kufuata sheria.
Kairuki alisema uwekaji vigingi 180 katika vijiji saba vya wilaya hiyo ambavyo ni Nyandage, Kenyamosabi, Masanga, Karagatonga, Nyabilongo, Kegonga na Gibaso ulianza rasmi Machi 23 hadi Aprili 27, mwaka huu, tayari limeondoa tofauti kati ya serikali, hifadhi na wananchi.
“Serikali ina lengo zuri na wananchi wake na ikumbukwe kuwa kazi ya askari wa uhifadhi ni kulinda wanyama waliopo katika hifadhi hiyo na siyo kulinda wananchi,” alisema Kairuki.
Aidha, Waitara aliiomba serikali kuanzisha mjadala wa kuwaelimisha wananchi na pia kuipitia ramani kwa lugha ya kiswahili na kufanya hivyo kutaweza kuwaondolea tafrani iliyopo baina yao na Hifadhi ya Serengeti.
Mmoja wa wananchi katika Kata ya Kegonga, Bhoke Nyamboge alisema kuwa eneo ambalo serikali imewapiga marufuku kuendeleza kilimo ni sehemu ambayo ilikuwa inawasaidia kuendeleza familia zao.