MKUU wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Meja General Fadhili Omari Nondo ametoa wito kwa kikosi maalumu kinachoenda kushiriki zoezi la kijeshi la ushirikiano imara kwa majeshi ya Afrika Mashariki kuhakikisha wanaiwakilisha Tanzania kwa kulinda amani na mshikamano.
Akikabidhi Bendera Ya Taifa kwa kikundi maalumu kinachoenda kushiriki zoezi la kijeshi la ushirikiano imara kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki alisema kuwa zoezi hilo linashirikisha vikundi mbalimbali vya majeshi hivyo Tanzania inawakilishwa na washiriki 81.
Alisema kuwa kikundi icho maalumu kinashirikisha washiriki ambacho kinaundwa na majeshi ya JWTZ ,Polisi ,uhamiaji, Magereza , zimamoto, Usalama wa Taifa, Wizara ya Mambo ya Nje,ofisi ya maafa kutoka kwa Waziri Mkuu pamoja na kituo cha Taifa cha kuratibu mapambano dhidi ya Ugaidi.
Alisema lengo la vikosi hivyo ni kushirikiana kwa pamoja namuna ya kupanga mikakati ya kutatua changamoto kwa pamoja juu ya kukabiliana na Ugaidi ,majanga,uharamia,pamoja na kujadili namna ya kulinda amani katika nchi za Afrika Mashariki .
“Kwa Niaba ya wakuu wa majeshi nchini Tanzania nimewakabidhi Bendera ya nchi ya Tanzania tunahitaji uwakishi mzuri na mahusiano bora ikiwa ni pamoja na kujifunza zaidi huku mkizingatia malengo ya mafunzo yaliyowapeleka huko kwa siku 14 nchini Rwanda ,nyie ni mabalozi wetu tunaomba mrudi mkiwa imara kwa uwakilishi mzuri ” alisema Nondo.
Mkuu wa vikundi washiriki wa zoezi la Ushirikiano Imara kwa nchi za Afrika Mashariki Brigedia Jenerali Mosses Gambos alisema kuwa washiriki kutoka nchi za Afrika Mashariki watakuwa 400 na mafunzo yatachukua siku 14 .