“DHANA ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ni huduma shirikishi kwa maana inaangalia maeneo ya afya bora, lishe kamili, ulinzi na usalama, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto tangu akiwa tumboni mpaka anapofikisha miaka minane.
“Ni mchakato mrefu na siku hizi zote za awali ndiyo msingi wa makuzi sahihi ya mtoto..ukichelewa tu hapa umeshampoteza mtoto huyu na ndipo unaweza ukajikuta sasa tunakuwa na watoto wenye changamoto nyingi.”
Ni sehemu ya hotuba aliyoitoa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Saidi Madito alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera kwenye uzinduzi wa kimkoa wa Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) uliofanyika jijini Mbeya, hivi karibuni.
PJT-MMMAM ni programu inayotekelezwa nchini ikilenga kuleta uchechemuzi ndani ya jamii katika malezi ya msingi ya watoto kupitia vipengele vya afya bora, lishe kamili, ulinzi na usalama, malezi yenye mwitikio na ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto katika umri wa tangu miaka sifuri hadi minane.
Kitaifa programu hii ya miaka mitano ilizinduliwa Desemba mwaka jana jijini Dodoma. Kwa Mbeya programu hii kimkoa ilizinduliwa Agosti 19 mwaka huu ikiwa ni kuonesha utayari wa mkoa kuanza kuitekeleza kwa ushirikishwaji wa wanajamii na wadau wote mkoani huo.
Kimsingi PJT-MMMAM imeyalenga zaidi maisha ya mtoto aliye na umri sifuri yaani tokea siku mimba inatungwa hadi atakapofikisha miaka minane. Kipindi kinachotajwa kuwa muhimu katika makuzi sahihi ya mtoto kwa kuwa ndicho kipindi pia muhimu katika ubongo wake.
Madito anasema matokeo chanya ya malezi stahiki kwa kipindi hiki ndiyo yenye kufanya jamii kuwa na watu wenye utimilifu ukubwani na kuiwezesha kuwa na maisha stahiki. Kutowekeza kikamilifu kwenye malezi ya awali ya mtoto ndiko kunasababisha baadhi ya jamii kuwa na watoto, vijana na watu wazima walio na changamoto nyingi na kuisababishia serikali kutumia nguvu nyingi kuwarekebisha.
Anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na uwepo wa watumiaji wa dawa za kulevya, makahaba na uwezo mdogo wa kufikiri kutokana na kukosekana kwa uchangamshi wakati ubongo wao ulipokuwa unajengeka.
“Serikali inatumia nguvu kubwa kulirekebisha kundi hili…maana tusipowarekebisha huku chini, huko juu ndiyo tunakutana na vijana wavuta bangi, wengine wako kwenye umalaya na wengine kwenye matukio mengine ambayo kwenye jamii hayana msaada,” anasema Madito.
Anasema ni muhimu wakati wadau wakizichambua na kuzipa kipaumbele afua za vipengele vinavyohimizwa kwenye programu hiyo kwa Mbeya wakajiuliza ni kwa nini licha ya uwepo wa fursa ya uzalishaji mkubwa wa mazao ya aina mbalimbali hususani ya vyakula bado mkoa uko kwenye hali mbaya ya udumavu.
“Tukielekea katika suala la lishe sisi Mbeya ni kati ya ile mikoa 10 ina hali isiyo nzuri kwenye utapiamlo. Sisi kwa takwimu zilizopo tuna asilimia 31.8 ya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ambao wana udumavu.
“Tafsiri yake ni nini? Unaweza ukawa na mtu mzima ambaye hana maamuzi..ukamlaumu kwamba huyu mbona hana maamuzi..lakini tatizo lilianzia huku alipokuwa mdogo. Unaweza ukawa na mtoto mzuri tu unamwona kwa umbile ni mzuri lakini mzembe hawezi kujituma vizuri tatizo lilianzia huku utotoni,” anasema Madito.
Anaongeza: “Tunapoangalia hizi takwimu si za kuzifurahia, sisi Mbeya tuna kila kitu tunafanya nini kuiondoa hali hii ya udumavu kwa asilimia hizi tulizonazo. Mungu ametupa kila kitu kwa nini tuwe kwenye kundi hilo.”
Anajiuliza pia kwanini vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinazidi kuongezeka, wananyanyaswa na kwa sasa kutokana na majukumu ya uzalishaji mali wazazi wanalazimika kuwaacha watoto wadogo na dada wa kazi au vituo vya kulelea watoto mchana na hivyo kukosa taarifa za uhakika za ulinzi na usalama wao.
Suala la malezi yenye mwitikio anasema ni eneo muhimu nalo kulifanyia kazi akisema ni huduma muhimu kwa mtoto aliye na umri mdogo ambaye mzazi au mlezi anahitajika kuwa karibu naye.
“Unaweza ukashangaa unalea mtoto baadaye anakuja kuwa mkatili sana, kumbe huku mwanzoni tangu alipokuwa mdogo mazingira uliyomjengea ni ya ukatili zaidi, mtoto unamtishatisha! Hapati furaha ya kutoka kwa mzazi au mlezi wake.
“Katika mazingira kama hayo sisi tunaamini kwamba mtoto wa namna hiyo haujamuwezesha vizuri kwa mwitikio chanya katika mazingira ya makuzi yake. Hivyo tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha watoto tulio nao kwenye jamii yetu wanapata huduma ya malezi yenye mwitikio chanya,” anasema.
Anasema jamii isipofanya vizuri kwenye eneo hilo, huduma zisipopatikana kwa ubora kutakuwa na kuyumba kwa maadili. Ni muhimu jamii ikatambua kuwa kijana au binti ili aje kuwa baba na mama bora lazima aandaliwe na ajengwe utotoni.
Anasema ili kutekeleza hilo ni muhimu wazazi na walezi kuepuka kisingizio cha kuwa na majukumu mengi na wawe karibu na watoto wao.
“Unafika hatua ya kutoa laana kwa watoto lakini tatizo lilianzia huku, mtoto hakuona upendo wa wazazi, na hivi sasa kwa teknolojia zetu za usasa na za uchumi hizi unatamani mtoto ashinde na toi la simu au kompyuta mama na baba muendelee na mambo mengine. Kwa hiyo mtoto anaziamini katuni anazoziona kwenye luninga au kompyuta zaidi kuliko wewe mzazi katika malezi,” anasema Madito.
Anaongeza: “Anaposhirikishwa zile hisia zinampelekea kujifunza kitu inategemea na elimu unayompa kwa kipindi hicho ni ya aina gani. Ujifunzaji wa awali wa mtoto una mchango mkubwa katika kukuza ubongo na afya ya mtoto ambapo katika kipindi hiki hukua kwa zaidi ya asilimia 90.”
Uchangamkiaji wa fursa za kuanzisha vituo vya mchana vya kulelea watoto wadogo unaonekana kukimbiliwa na wadau wengi nchini akasema ni muhimu kuangaliwa kwa umakini zaidi.
“Kwa takwimu tulizonazo kuna vituo 5,274 vya kulea watoto mchana nchi nzima. Kwa Mkoa wa Mbeya vipo vituo 243. Na mara nyingi watoto wanaopelekwa ni wale wadogo mpaka wa miaka mitano. Kama nilivyosema sisi wazazi tuko bize tunakimbizana na shilingi na hiki na kile, je, tumefuatilia kule tulikowapeleka watoto wanajifunza nini? Wanahudumiwa vipi? Kwenye vituo waliko kuna watu sahihi wa kuelezea kile kinachotakiwa kwa watoto hawa,” anahoji Madito.
Anasema matokeo ya hayo ni mtoto kurudi nyumbani likizo akikosa upendo na wewe. “Ukimwambia mwanangu usifanye hivyo anakujibu madam alituambia tufanye. Sasa unaanza kuona kasoro. Hivyo hata kwenye vituo vilivyopo kuna jambo la msingi tunalopaswa kulifanya sisi la kuhakikisha kile kilichopo kina mchango chanya katika malezi na makuzi ya mtoto huyu.”
Anasema yasipofanyika hayo vituo hivyo vinaweza kutumika kutengeneza bomu kwa siku zijazo. Vipo vingi lakini kwa mahitaji yaliyopo yawezekana havitoshi maana bado kuna watoto wanaonekana kurandaranda mitaani na wengine wapo kwenye mazingira magumu lakini ni muhimu wadau wakavifuatilia si kwa kuwakatisha tamaa walezi hao bali watoto wapate haki stahiki ya kujifunza na ya malezi.
Kwa mujibu wa Madito, PJT-MMMAM imekuja katika kipindi ambacho ni sahihi zaidi, ni sehemu ya utekelezaji wa sera na miongozo inayoletwa na serikali katika kuimarisha jamii.
Sera ya Mtoto ya mwaka 2008 na Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2019 na Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2016 zote ni nyezo za kuwezesha wadau wote kumjengea mtoto mazingira sahihi ya ukuaji.
Akitoa maelezo ya Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Salome Francis aliutaja Mkoa wa Mbeya kuwa wa saba kuzindua PJT-MMMAM kimkoa tangu ilipozinduliwa kitaifa Desemba mwaka jana.
Salome alihimiza mikoa iliyosalia kuhakikisha wanashirikisha wadau muhimu wote kwenye uzinduzi wa programu hiyo ili kuwezesha kuwepo kwa uelewa wa pamoja kwenye utekelezaji wake na kuwezesha matokeo chanya yanayotarajiwa.
Meneja mradi wa Shirika la Kihumbe lililopewa jukumu na mkoa huo la uchechemuzi wa programu hiyo kupitia Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto nchini (TECDEN), Jeremiah Henry alisema mafanikio ya uzinduzi huo yametokana na ushirikishwaji wa pamoja baina ya sekretarieti ya mkoa na wadau wengine yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali.
Naye Ofisa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la CRS, Neema Haule pamoja na kupongeza uwepo wa viongozi katika ngazi ya mkoa walio na upeo mkubwa juu ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto, alisema kufanikiwa kwa programu hiyo kutatokana na kila mmoja kwa nafasi yake kutambua kuwa analo jukumu la kuwa karibu na watoto.