Mbinu zahitajika wenye mitaji midogo vijijini

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka taasisi za utafiti na zinazotoa mafunzo ya misitu wakiwemo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuendelea kubuni mbinu na teknolojia rahisi kwa ajili ya wananchi wa vijijini wenye ujuzi na mitaji midogo.

Lengo ni kuwawezesha kutumia ipasavyo rasilimali za misitu kwa njia endelevu za kiuchumi na yenye manufaa kwa taifa na vizazi vijavyo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Omary Kipanga amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Jubilii ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa ndaki ya mafunzo ya misitu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Kipanga amesema nafasi ya sekta ya misitu katika maisha ya binadamu na katika maendeleo ya taifa  ni kubwa kama ambavyo utafiti unavyoeleza kuwa eneo la misitu kwa Tanzania ni hekta milioni 48 ambalo ni sawa na asilimia 55 za ardhi yote ya Tanzania Bara.

Rasilimali za misitu zinatoa fursa za ajira kwa Watanzania na wasio kuwa Watanzania zaidi ya 3,000,000 upatikanaji wa maji, makazi na malisho ya wanyamapori, uhifadhi wa udongo na baioanwai, urutubishaji wa hewa ukaa pamoja na maendeleo ya utalii wa kiikoloji,”alisema Kipanga.

Naibu Waziri Kipanga amesema  umuhimu wa sekta ya misitu huonekana pia katika maeneo yaliyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Maendeleo  Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Amesema katika kipindi cha mika 50 tangu kuanzishwa kwa kitivo cha mafunzo ya misitu, wanyamapori na utalii katika chuo hicho, wataalam wa misitu 2,630 wamehitimu mafunzo hayo kwa ngazi mbalimbali ambao wanasimamia rasilimali za misitu ndani nan je ya Tanzania.

“Kwa hapa nchini wataalam hawa wamesezesha kutengwa kwa hekta milioni 45 ya hifadhi za misitu pamoja na uanzishwaji wa hekta 500,000 za mashamba ya misitu ya kibiashara,” amesema Kipanga.

Naibu Waziri huyo amekitaka chuo hicho kione umuhimu wa kuwa na mikakati thabiti ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho ,Profesa Raphael Chibunda amesema menejimenti na wafanyakazi wa kitivo cha misitu wanakitazama kitivo hicho kwa jicho la kipekee .

Profesa Chibunda amesema mkakati uliopo ni kukifanya kuwa kitivo cha umahiri kutokana na SUA kuwa chuo kiongozi kwenye sekta ya misitu ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Habari Zifananazo

Back to top button