Mbogwe wapewa somo kuchuja viongozi

GEITA; WAKAZI wa Jimbo la Mbogwe mkoani Geita, wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudadisi na kuchuja sifa za viongozi bora wanaofaa kuelekea uchaguzi mkuu 2025.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbogwe, Pius Lukaga ametoa wito huo kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Nyakafuru wilayani humo.

Lukaga amesema kwa kutumia katiba ya Tanzania, wananchi wanayo Mamlaka ya kuchagua diwani, mbunge na Rais mwenye uwezo na anakidhi vigezo vya kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

“Mwaka huu ni wa kutembea kifua mbele, huku ukidunda na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa nyinyi mwaka huu (2025) ndio mtaajiri watu wengi.

“Watakuja wanaotafuta udiwani, mtakaa mbele na mafaili kuwachuja, mpate kiongozi atakayesimama kwa niaba yenu, msipate kiongozi ambaye yeye matakwa yake ni kujinufaisha mwenyewe”, amesema Lukaga.

Aidha Lukaga amewaomba wananchi kutumia vizuri fursa ya mabadiliko ya sheria ya uchaguzi iliyozaa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili kufanikisha uchaguzi huru na haki kwa kila mmoja.

“Ukiangalia sheria namba 02, inasema badala ya kuwa na Tume ya Uchaguzi, sasa tuna Tume Huru ya Uchaguzi, ambapo mwenyekiti na wajumbe wake wamelindwa kikatiba hamna mtu wa kuwabugudhi”, amesisitiza.

“Kwa nafasi ya urais, ukiangalia kifungu cha 32(2) endapo atagombea atapingwa, kwa upande wa mbunge kuna kifungu cha 54 (2) endapo atagombea peke yake kutakuwa na kura ya ndiyo au hapana.

“Kwa upande wa madiwani kifungu cha 67 (2) endapo atagombea peke yake kutakuwa na kura ya ndiyo au hapana, hiyo ni kazi kubwa ambayo imefanyika kuleta marekebisho ya sheria ya uchaguzi”, amesema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button