Mbunge afanikisha ukarabati madarasa Lupanga

MBUNGE wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Morogoro, Norah Mzeru ametoa mifuko 100 ya saruji na kuwezesha ukarabati mkubwa wa vyumba vya madarasa chakavu katika shule ya sekondari Lupanga,Manispaa ya Morogoro.

Hatua hiyo imewawezesha wanafunzi wa shule hiyo kupata muda wa kusoma wakiwa kwenye mazingira mazuri zaidi.

Mkuu wa shule hiyo, Flora Ndunguru amesema uongozi wa shule unampongeza mbunge huyo kwani amekuwa na msaada.

Ndunguru amesema shule hiyo imejiwekea mikakati ya kuendelea kukuza taaluma na kufundisha kwa bidii ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani ya taifa na hivyo kuijengea sifa Manispaa ya Morogoro na mkoa kwa ujumla.

Kutokana na mkakati huo uongozi wa shule hiyo umemwomba awezeshe kufanikisha ujenzi wa uzio wa shule kwa lengo la kuongeza ulinzi kwa wanafunzi na mali za shule.

Kwa upande wake mbunge Mzeru ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu ambapo kata ya Kilakala ni miongoni mwa wanufaika na miradi hiyo.

Pia ameuhakikishia uongozi wa shule hiyo kuwa atasaidia kujenga uzio wa shule kwa kutoa ahadi ya kuchangia Sh 500,000 kikiwa ni kianzio huku akiwaomba wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuchangia fedha ili uzio ujengwe kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na mali zote zilizopo shuleni.

Diwani wa kata ya Kilakala, Marco Kanga amesema awali shule ya sekondari Lupanga ilikuwa na vyumba vya madarasa 10 na baada ya kuingia kwa serikali ya awamu ya sita imewezesha fedha na kujengwa madarasa zaidi na kuifanya iwe na jumla ya madarasa 23.

Habari Zifananazo

Back to top button