Mbunge Malinyi akumbushia miundombinu ya barabara

DODOMA:MBUNGE wa Jimbo la Malinyi Dk Mecktridis Mdaku ameiomba Wizara ya Ujenzi kuendelea kuzingatia changamoto za kijiografia na mazingira katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, akisema maeneo yenye mvua nyingi na mafuriko yanahitaji mbinu maalumu za ujenzi wa kudumu.
Akichangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Dk Mdaku amempongeza Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya miundombinu nchini, akibainisha kuwa uwekezaji huo umeongeza uhusiano wa kiuchumi kati ya mikoa na kuboresha huduma kwa wananchi.
Amesema Jimbo la Malinyi linakabiliwa na changamoto za mara kwa mara za uharibifu wa barabara kutokana na mvua kubwa na mafuriko, hali inayohitaji ujenzi wa miundombinu yenye ubora wa kudumu ili kuhimili mazingira hayo.
Aidha ameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Kuroka – Ifakara – Lupilo – Mtimbira, akisema ni muhimu katika kuunganisha shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya wakulima katika ukanda huo.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuboresha barabara ya Malinyi – Lumbecha – Londo – Namtumbo ili kuimarisha mawasiliano ya kikanda kati ya Mikoa ya Morogoro na Ruvuma, hatua itakayochochea biashara na uwekezaji.
Katika hatua nyingine, ameiomba serikali kuzingatia umuhimu wa daraja la mto Fulwa pamoja na mradi wakivuko cha Kikove, akieleza kuwa miradi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi hawakatiziwi huduma za msingi wakati wa vipindi vya mvua.
Amesema changamoto za miundombinu katika maeneo ya mafuriko zinahitaji mipango ya muda mrefu na uwekezaji wa kimkakati ili kuhakikisha huduma za kijamii na kiuchumi hazisumbuliwi na hali ya hewa.
Pia, amepongeza juhudi za serikali katika sekta ya ujenzi, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na viongozi wa maeneo husika ni muhimu katika kupata suluhisho la kudumu la changamoto za miundombinu.



