MBUNGE wa Bunge la Tanzania, Anatropia Theonest ameibuka mshindi wa riadha kwa wanawake katika mashindano ya mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayoendelea jijini Mombasa nchini Kenya.
Anatropia ameshika namba moja katika mbio za mita 1500 akiwashinda wapinzani kutoka Bunge la Uganda, Kenya, Rwanda na Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Vilevile katika mbio za mita 400, aliibuka mshindi kwa kushika nafasi ya kwanza akimpita mpinzani wake kutoka Bunge la Uganda.
Aidha, katika mbio za mita 100 mbunge Condesta Sichwale alishika nafasi ya tatu huku, Saada Mansour Hussein akishika nafasi ya tano katika mbio hizo.
Katika mbio za wanaume mita 100 mbunge Jaffar Chege aliibuka mshindi wa tatu nyuma ya wapinzani wake kutoka Bunge la Kenya na Uganda.
Kwa upande wa mbio za kupokezana vijiti, Timu ya Tanzania ya Riadha wanawake iliibuka mshindi wa pili huku riadha wanaume wakiibuka mshindi wa nne.
Kwenye mchezo wa kamba, Timu ya Tanzania Wanaume ilijizolea pointi 2-0 baada ya kuiburuza timu ya Wanaume ya Bunge la Kenya.
Kwa upande wa Timu ya Wanawake ya Kamba Bunge la Tanzania wameibuka kidedea kwa pointi 2-0 baada ya kuigaragaza Timu ya Wanawake ya Bunge la Kenya.
Nayo timu ya Wanawake ya Mpira wa Wavu ya Bunge la Tanzania imejinyakulia pointi za mezani baada timu pinzani ya Bunge la Sudani Kusini kushindwa kufika uwanjani.