Mchezo wa vihunzi kuanzishwa nchini
WADAU wa michezo wapatao 50 kutoka mataifa mbalimbali wamefundwa sheria za mchezo wa vihunzi watakazotumia kusimamia na kuanzisha mchezo huo ambao ni mpya Tanzania.
Miongoni mwa nchi zilizoshiriki katika mafunzo hayo yanayofanyika Dar es Salaam chini ya mwenyeji Scope Event ni Tanzania, Zanzibar, Rwanda, Kenya na Denmark.
Mkufunzi kutoka Chama cha Kimataifa cha Mchezo wa Vihunzi (World Obstacle) Nayibe Statia ameiambia Dailynews Digital kuwa amekuja kutoa mafunzo lengo ni kuona mchezo huo unaanzishwa na kuinuka.
“Shauku yangu ni kuona baada ya mafunzo haya hatua kubwa ipigwe kwa kuendeleza mchezo huu na kuhakikisha wanajua maana ya mchezo na sheria zake, Napenda kuiona Tanzania inashiriki mashindano ya Afrika na Dunia hapo baadaye,” alisema Mkufunzi huyo kutoka Visiwa vya Caribbean.
Amesema amevutiwa na Tanzania kwa kuwa ni watu wakarimu, na anauona mchezo huo ukikua kutokana na kuwa ni nchi iliyobarikiwa rasilimali na mazingira mazuri kwa ajili ya michezo.
Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Scope Event Abdallah Chapa amesema mwaka 2019 Chama cha Dunia ha Vihunzi kilifanya mashindano kwenye Mlima Kilimanjaro na wageni waliweka rekodi wakaona na wao kuna haja ya kuanzisha michezo hiyo nchini.
Chapa amesema michezo ya vihunzi ipo mingi ndani yake kama riadha za kuvuka maji, kuruka, kuendesha baskeli milimani, mbio za vyombo vya maji na michezo mingine mingi na mara nyingi hufanyika katika mazingira yenye vivutio vya utalii.
“Michezo hii ina faida kubwa kuitangaza nchi, unatangaza utalii kwasababu watu wanakimbia katika maeneo yenye utalii kutoka nchi moja kwenda nyingine. Na sisi tunataka tutumie mchezo huu kusaidia kukuza kiuchumi, unatengeneza fursa za ajira na biashara,”amesema.
Mwanasheria wa masuala ya michezo Frank Pius amesema mafunzo hayo yamekuja kubadilisha uelewa juu ya mchezo mpya, itawasaidia hasa vijana kupata ajira mpya, kuepusha watu kukaa kwenye magenge ya uovu.
View this post on Instagram