‘Mchumba’ amjeruhi mwenza, mtoto

MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha Nyahera, Kata ya Tai, Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Night Mchama (27) na mwanawe mwenye umri wa mwaka mmoja wamejeruhiwa kwa visu na mapanga.

Inadaiwa mchumba wa Night, Jacob Ngoro ndiye aliyewajeruhi na chanzo ni mama huyo kukataa kuishi na Jacob bila ya kulipiwa mahari.

Tukio hilo limetokea Juni 7, mwaka huu wakati Jacob alimvamia Night nyuma ya nyumbani kwao na kumtaka waondoke na kwenda kuanza maisha mapya.

Inadaiwa Night alishambuliwa kwa visu katika maeneo ya bega la kushoto na kulia zaidi ya mara mbili, kisha katika mapaja.

Baada ya Night kuanguka, Jacob alitoa panga alilokuwa amelificha ubavuni na kumkata tumboni na kumkita nalo tumboni na baadaye alimgeukia mtoto wao na kumshambulia kwa visu maeneo ya mabega, mapaja na tumboni.

Akizungumza akiwa hospitalini, Night alidai Jacob alifikia hatua hiyo baada ya kukataa kutoroka naye kama walivyowahi kufanya walipokutana mwaka 2021, alikuwa akimtishia maisha mara kwa mara na alikuwa akimpiga alipokataa kumtii.

“Niliomba msaada kwa kupiga kelele, ndipo baba yangu alipotokea na nikamuomba anisaidie kutoa panga lililokuwa limechomekwa tumboni,” alisema.

Baba wa Night, France Nyerere alisema alipofika eneo la tukio alimkuta binti yake akivuja damu huku akimwita kwa kumtaka kutolea panga alilokitwa tumboni.

Alieleza kuwa kabla ya tukio hilo familia ilimshauri kurudi nyumbani kutokana na mazingira ya familia aliyokuwa akiishi, ambayo ilihusishwa na vitendo vya kishirikina.

“Mwezi Mei, mwaka huu baba mzazi wa Jacob alifariki dunia kwa kujinyonga katika mazingira ya kutatanisha, jambo lililonifanya kuwa na wasiwasi juu ya hatima ya binti yangu,” alidai Nyerere.

Daktari wa zamu katika Kitengo cha Dharura Hospitali ya KMT Shirati, Chrispin Msabi alisema walimpokea Night akiwa katika hali mbaya na walimpeleka chumba cha upasuaji na kubaini alikuwa amechanwa utumbo mwembamba na mshipa mkubwa wa damu.

Alisema walilazimika kuukata utumbo mara mbili ili kuuunganisha tena kabla ya kumpeleka chumba cha wagonjwa mahututi kwa uangalizi wa karibu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyahera, Joseph Mgasausi alithibitisha tukio hilo, na kusema walitoa taarifa Kituo cha Polisi Shirati na askari walifika na kuwachukua majeruhi hadi hospitali. Wanaendelea na juhudi za kumtafuta mtuhumiwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button