MCT: Serikali iongoze nguvu ulinzi wa wanahabari

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura amesema kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2024 Oktoba waandishi wa habari 316 walipatwa na madhila mbalimbali yakiwemo kukamatwa, vitisho na kutekwa.

Hayo yemesemwa leo Novemba 2, 2024 katika Maadhimisho ya Kimataifa ya Kupinga Dhuluma na Ukatili dhidi ya waandishi wa habari yaliyofanyika mkoani Singida nakuandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Sungura amesema Serikali ya Tanzania Ina kila sababu ya kuongeza nguvu ya kuwalinda waandishi wa habari dhidi ya Madhila.

Advertisement

Sungura amesema Mwaka 2022 madhila 19 yalirekodiwa, mwaka 2023 madhila 23 na mwaka 2024 hadi
leo madhila 33yamerekodiwa.

“Madhila yaliyopo ni waandishi wa habari ukamatwa, kupewa vitisho, vyombo vya habari kupewa onyo, kufungiwa kufanya kazi, kuingilia uhuru wa mahakama na kuahirisha kipindi kwenda hewani”amesema Sungura.

Sungura amesema kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji za UNESCO kuhusu ukatili dhidi ya waandishi wa habari kiwango cha ukatili ni kikubwa kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2024.

Ameongeza na kueleza kuwa zaidi ya waandishi 1700 wameuwawa duniani kote na kesi za mauaji hayo asilimia 90 hazijatatuliwa.

Sungura amesema kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya waandishi wa habari wasio na mipaka (RSF) amesema Tanzania imepanda katika viwango vya Uhuru wa habari kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 Hadi nafasi ya 97 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya amesema suala la Madhila kwa waandishi kimeanza kufanyiwa kazi kwa vitendo na waratibu wa kila Klabu katika mikoa walikwisha pewa Mafunzo ya namna ya kuyatolea taarifa.