Messi afikiria kumaliza soka lake Marekani
MAREKANI – MSHAMBULIAJI Lionel Messi amesema anakusudia kumaliza soka lake kwenye klabu ya Inter Miami lakini bado hajapanga kustaafu.
Mshindi huyo mara nane wa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa dunia mwenye umri wa miaka 36, alijiunga na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani akitokea Paris Saint-Germain ya Ufaransa wakati wa majira ya kiangazi ya msimu uliopita.
Nyota huyo alikuwa na kipindi kizuri wakati akiitumikia Barcelona ambapo alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne na mataji 10 ya La Liga.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Argentina ana mkataba na klabu hiyo ya Marekani unaofikia kikomo mwakani ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
“Mpaka sasa nadhani hii itakuwa klabu yangu ya mwisho,” alisema mshambuliaji huyo. “Siko tayari kuachana na soka hata hivyo,” alisema.
SOMA: Droo kufuzu Afcon Morocco 2025 kupangwa Julai 4
Messi hachezi kama mtu aliyeelekeza jicho moja kwenye kustaafu, msimu huu amefunga mabao 12 na kutengeneza mengine 13 kwenye mechi 12 za Ligi Kuu soka Marekani.
Anatazamia kuiongoza timu ya taifa ya Argentina kutetea taji la Copa Amerika waliloshinda mwaka 2021 baadaye mwezi huu.
Mashindano ya Copa America yanafanyika Marekani nchi ambayo Messi imekuwa kama nyumbani kwake kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.