Mfanyabiashara atoweka akifuatilia kontena lake

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro

MFANYABIASHARA, Daisle Ulomi ametoweka alipokuwa akifuatilia kontena la bidhaa zake katika Bandari Kavu, Mbagala mkoani Dar es Salaam.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilieleza hayo jana kupitia taarifa yake kwa umma na kusema kuwa Desemba 12, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke walipokea taarifa ya mfanyabiashara huyo kutafutwa na familia yake baada ya kutorudi nyumbani tangu Desemba 11, mwaka huu.

Inadaiwa kuwa hakuonekana tangu alipoenda kazini siku hiyo na kuwa alionekana akitoka ofisini kwake Sinza Kijiweni majira ya saa 6:00 mchana kuelekea Mbagala, Bandari Kavu alikodai anaenda kukagua kontena la bidhaa zake baada ya kuitwa na watu aliodai wanashughulikia kontena hilo bandarini.

Advertisement

Ilielezwa kwamba alikuwa akitumia pikipiki namba MC 415 DQC aliyokuwa akiendesha mwenyewe.

Jeshi la Polisi lilieleza kuwa ufuatiliaji wa taarifa hiyo unafanywa kwa kushirikiana na ndugu ili kujua mtu huyo yupo wapi.