Mfumo wa uanagenzi kufungua ajira kwa vijana

DAR ES SALAAM: Wadau wa maendeleo ya ujuzi nchini wameeleza kuwa kuimarishwa kwa mfumo wa uanagenzi (apprenticeship) unaozingatia mwongozo wa kimataifa wa mafunzo ya uanagenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.

Kauli hiyo imetolewa katika kikao kazi kilichoandaliwa na ILO kupitia Programu ya Ujuzi ya Dunia kwa ufadhili wa Norway, kilicholenga uthibitishaji wa mpango wa utekelezaji wa mafunzo ya uanagenzi (Apprenticeship Road Map). Kikao hicho kilifanyika mkoani Morogoro na kuwakutanisha wadau kutoka taasisi za elimu, vyuo vya ufundi, serikali pamoja na sekta binafsi kujadili namna ya kuboresha mfumo wa mafunzo kwa vitendo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mshauri wa Masuala ya Ukuzaji Ujuzi kutoka ofisi ya ILO Pretoria, Albert Okal, amesema warsha hiyo imelenga kutathmini namna mfumo wa uanagenzi unavyoendeshwa Tanzania na jinsi unavyoendana na mwongozo wa kimataifa uliowekwa na ILO pamoja na wanachama wake.

Okal amesema uchambuzi wa mitaala uliofanywa umebaini kuwa mfumo wa uanagenzi nchini bado haujafikia kiwango kinachotarajiwa.

“Baadhi ya taarifa zinaonesha kuwa uanagenzi bado haujawa sehemu kubwa ya mfumo wa mafunzo ya amali kama ilivyo kwa programu nyingine za elimu ya ufundi. Tunatarajia ripoti hii itatusaidia kubaini maeneo yanayohitaji maboresho,” amesema Okal.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk. Bakari Ali Silima, amesema mfumo wa uanagenzi ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha wahitimu wanapata ajira kutokana na kuandaliwa kulingana na mahitaji ya soko la kazi na viwanda.
“Mafunzo ya uanagenzi yanahitajika sana katika taasisi zetu za elimu, hasa vyuo vikuu.

Tukifanikiwa kutoa mafunzo haya kwa ufanisi, tutasaidia kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu masomo yao. Pia suala la vijana kuwa na ujuzi zaidi ya mmoja linapaswa kupewa kipaumbele,” amesema Dk. Silima.

Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, Daudi Simbeye, amesema serikali imejipanga kuhakikisha mfumo huo unakuwa sehemu muhimu ya kuwasaidia vijana kupata ajira na kujiajiri.

Amesema serikali kupitia programu ya utambuzi wa ujuzi ijulikanayo kama SAMIA inaendelea kuwasaidia vijana waliopata ujuzi katika sekta isiyo rasmi kutambulika rasmi kwa kupatiwa mafunzo na vyeti vinavyowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Dennis Assey, amesema kupitia warsha hiyo, ILO imewasilisha ripoti ya tathmini iliyochunguza hali halisi ya mfumo wa uanagenzi Tanzania kwa kuzingatia Recommendation 208.

Assey amesema serikali itaendelea kushirikiana na ILO katika kuimarisha mfumo huo kupitia Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi, ambapo zaidi ya vijana 5,000 wanaendelea kupata mafunzo ya uanagenzi katika vyuo 46 nchini.

“Katika mwaka wa fedha 2025/26, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini imeendelea kutekeleza programu ya taifa ya ukuzaji ujuzi.

Eneo mojawapo ni mafunzo ya uanagenzi ambapo zaidi ya vijana 5,000 wanaendelea kujifunza katika vyuo 46 nchini. Tunawahimiza vijana kufuatilia na kutumia fursa hizi zinazotangazwa kila mwaka,” amesema Assey.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button