Mganga Mkuu Mbogwe kuchukuliwa hatua
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI Adolf Ndunguru kumchukulia hatua za kinidhamu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Dk Theopister Elisa.
Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Tamisemi, Nteghenjwa Hosseah imesema kuwa Mchengerwa ametoa maagizo hayo kwa kile alichoeleza kuwa Mganga Mkuu huyo ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma za afya kwenye halmashauri hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mchengerwa kupokea taarifa ya utendaji kazi usioridhisha katika usimamizi wa miradi ya afya pamoja na shughuli mbali mbali za Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kwenye halmashauri hiyo ya Mbogwe.
Aidha, ameelekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa mujibu wa kanuni ya 42 ya Kanuni ya Utumishi wa Umma za mwaka 2023 inayoainisha adhabu kwa mtumishi aliyekiuka kanuni hiyo kuwa ni kushushwa cheo, kukatwa mshahara kwa asilimia 15 kwa muda usiopungua miaka mitatu ama kufukuzwa kazi.
Pia amewataka Wakuu wa Idara ya Afya kushirikiana na Wakurugenzi kote nchini kuhakikisha kwamba ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya unaendelea nchini kote unasimamiwa kikamilifu ili thamani ya fedha ionekane.
Aidha, kwa wale waliomaliza ujenzi wahakikishe wanakamilisha taratibu za usajili wa vituo hivo haraka ili vianze kutoa huduma kwa wananchi.