Mgogoro wa mpaka uliodumu miaka 15 wamalizwa

ARUSHA: Mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Ziwa Manyara uliodumu zaidi ya miaka 15 kijiji cha Buger wilayani Karatu umepata mwarobaini wake baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella kuamuru alama za mipaka kuwekwa mara moja kuzunguka hifadhi huku nyumba tatu za wananchi zikiachwa pamoja na kisima cha maji.

Akitatoa maazimio ya mgogoro huo kijijini hapo mbele ya wananchi hao, Rc Mongella amesema serikali imeamua kuacha nyumba tatu za wananchi zilizoingia ndani ya hifadhi hiyo ya ziwa hilo pamoja na kisima cha maji sawa na eneo la ekari 8.3.

Advertisement

Pia ameagiza alama za mipaka kuwekwa mara moja katika hifadhi hiyo na kuacha barabara kidogo ili wananchi wajue mwisho wa mpaka kati ya kijiji na hifadhi hiyo

“Alama za mipaka kuzunguka hifadhi hii ziwekwe mara moja na kuanzia sasa mgogoro umeisha nyumba zilizoingia ndani ya hifadhi tatu pamoja na kisima zimeachwa sasa ni wajibu wenu wa kuheshimu mpaka huu unaowekwa na baada ya hapa mtu akiingia hifadhini au mifugo ikiingia kule hifadhini wakati mpaka wenu umejulikana hatua zitachukuliwa”

Awali Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Eva Mallya amesema walishirikiana na wataalam wa ardhi na wananchi kwaajili ya kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo sanjari na uwekaji wa alama (bicon) utaanza mara moja ili kila mtu ajue umuhimu wa uhifadhi na alama zilizowekwa.

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo, Safari Michael na Samson Bayo wanasema hawana tena mgogoro baina ya hifadhi na wananchi hao kwakua sasa alama zimewekwa na wananchi wamekubali hivyo watapenda kuona amani ikitawala katika eneo hilo na kuiomba serikali kutafuta mwekezaji ili waweze kupata miradi ya maendeleo na wananchi kunufaika na miradi itakayobuniwa.