Miaka 36 ya Tamwa na Levina Mukasa

*yakata minyororo ya ukatili

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) mwezi huu wa Novemba kimetimiza miaka 36 tangu kilipoanza harakati zake za kukata minyororo ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa matukio makubwa ambayo TAMWA itakumbwa nalo ni la kuendesha kampeni kubwa ya kupinga ukatili wa kijinsia baada ya kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Levina Mukasa.

TAMWA iliendesha kampeni hiyo mwanzoni mwa miaka ya 1990, “Walitishwa” hasa baada ya kuchukua hatua ya kutoa toleo maalum la gazeti la mwanamke maarufu ‘Sauti ya Siti’ ambalo linamilikiwa na chama hicho likiangazia kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Levina Mukasa aliyefariki Februari 7, 1990.

Picha ya Levina ambayo ilichapishwa na TAMWA ilisambaa katika vyombo vya habari vya Tanzania na Pan-African mwanzoni mwa miaka hiyo ya 1990.

Picha iliashiria kifo cha Levina na tatizo la unyanyasaji dhidi ya wanawake nchini Tanzania, kielelezo hicho kilikuja kutoa msukumo wa harakati za kitaifa dhidi ya ukatili wa kijinsia na kimetumika kama ukumbusho wa gharama za unyanyasaji wa kijinsia nchini.

NINI KILIMPATA LEVENA?
Katika toleo la Sauti ya Siti lililochapishwa mwanzoni mwa 1990 na Mwanahabari Chemi Che-Mponda alielezea kushindwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kujibu malalamiko ya mara kwa mara ya Levina ya unyanyasaji wa kijinsia na kifo chake cha kujiua.

Shangazi yake Levina na mhadhiri wa chuo kikuu, Dk. V. K. Massanja, alieleza kwamba matatizo ya mpwa wake yalianza alipokataa kuhudhuria dansi ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza iliyofanyika kwenye hoteli ya Silversands ambapo alikataa kwenda na mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Kitivo cha Uhandisi (Engineering) aitwaye Mark Victor.

FUJO

Levina alienda dansi hiyo na rafiki zake. Victor alipomuona alimtaka warejee pamoja na akalalamika kwa nini alidhubutu kwenda kwenye dansi na watu wengine wakati alikataa kwenda naye.

Levina alikataa kuondoka naye na Victor akamvuta gauni, rafiki zake walijaribu kumtetea na papo hapo ugomvi ukaanza. Baadhi ya marafiki wa Victor wanaojita “Engineers” [Wahandisi] [kundi lililokuwa maarufu sana UDSM maarufu PUNCH walimsaidia Victor. Kundi jingine lililojulikana kama “insiders” walimsaidia Levina. Hatimae, baada ya kushindwa Wahandisi waliondoka kwenye dansi, lakini huo haukuwa mwisho wa matatizo ya Levina.

Waliporejea kwenye dansi mgogoro mwingine ulizuka kati ya Victor na kundi lake na Levina na rafiki zake. Walipofika kwenye mabweni yao, Victor alikuwa akimsubiri ndipo ikawa usiku mzima kutupiana matusi.

Asubuhi na mapema Levina alipeleka malalamiko MUWATA [Serikali ya wanafunzi] uongozi ambao ulisulihisha tatizo hilo. Victor aliomba radhi na akadai kuwa alikuwa amelewa.

Siku iliyofuatia, tukio la Silversands lilipanchiwa. Michoro ya Punch haikumwonyesha jina lake lakini kwa kutoa namba yake yakusajiliwa ilidhihirisha kuwa michoro inayofuatia angekuwemo.

Baadhi ya wanafunzi wa kiume walimwendea Levina na kumwambia kuwa alikuwa kwenye kundi la PUNCH. Walimtishia kumpanchi iwapo angekataa kufanya nao mapenzi. Aliwakatalia na akakosa raha sana. Mmojawapo wa wanafunzi hao alikuwa Omari Saloti, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Uhandisi.

Dk Masanja alisema kuwa yeye (Levina) ndiye alimweleza yaliyotokea. Dkt. Masanja alisema kuwa alimweleza Levina kuhusu uzoefu wake na mambo ya PUNCH alipokuwa mwanafunzi na jinsi alivyoweza kuyapuuza.

Alisema kuwa Levina alionyesha kupata ujasiri na akafikiria kuwa mambo yamekwisha. Marafiki wa Levina waliambiwa kuwa wangepanchiwa iwapo wangeonekana wakiandamana naye. Alitengwa.

Maelezo machafu yalitolewa na maandishi yaliandikwa dhidi ya jina lake katika kila orodha ya majina na lake likiwemo.

Usiku Februari 3 mwaka huo saa 7.30 wakati Levina alipokuwa kitandani akijisomea alisikia mlango ukigongwa. Kabla hajajibu, mlango ulifunguliwa na Omari Saloti aliingia kwa nguvu chumbani. Walipigana.

Levina alimng’ata mkono naye alimpiga ngumi za mashavuni na kwenye matiti.

Levina alikimbia akiwa amevaa gauni ya kulalia tu na akajificha kwenye kichaka kilichoko nje ya bweni wakati Saloti akiwa bado anamnyemelea. Aligonga nyumbani kwa mlinzi, ambaye alimsindikiza hadi chumbani kwake na akasubiri kwa muda nje.

Mnamo Februari 7,1990, Levina alikatisha maisha yake kwa kumeza vidonge vingi vya klorokwini (vinavyotumika kutibu Malaria).

Swali linabaki, “kwa nini alifanya hivyo?” Karibu kila mwanafunzi wa kike aliyesoma katika kampasi kuu ya Chuo Kikuu (inayojulikana sana kama Mlimani) atakuwa amenyanyaswa kijinsia katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita. wamekuwa wakidhihakiwa, kutishiwa kijinsia au kuvamiwa papo kwa hapo na kubakwa.

LENGO LA PUNCH KUDHALILISHA WANAWAKE

Inasemekana kuwa Saloti alitaka kumbaka, wakati wengine wanasema alimbaka.

Wanasema Levina alikataa tu kusema. Hata hivyo Saloti alikuwa amemtishia Levina kuwa angembaka na kumwibia vitu vyake.

Asubuhi iliyofuatia, mlinzi alisema kuwa alizungumza na Saloti na akasema alikuwa “Amelewa” wakati huo.

Levina pia aliripoti tukio hilo kwa Meneja wa Bweni, ambaye alizungumza na Saloti. Alisema kuwa Saloti alimwambia kuwa alifunguliwa mlango na Modesta mwenzake Levina ambaye walikuwa wakiishi naye chumba kimoja. Modesta, alikanusha madai hayo kwani yeye ameolewa na kila mwisho wa juma huwa nyumbani na familia yake.

Dk Masanja alisema alimpa barua Levina na kumwelekeza kwa Mshauri wa wanafunzi, Dkt. Biswalo ambaye alikuwa akienda kwenye Mkutano wa Baraza hivyo naye alimuelekeza kwa Mama Rajabu.

Waliitisha jalada la Meneja wa Bweni/Mlinzi lakini halikuwa na chochote. Levina alifariki jioni ya Februari 7, 1990.

Inaonekana kuwa kundi la Punch ni mabingwa wa vita vya kisaikolojia na wamefanikiwa lengo lao kinyume cha matarajio yao kwa kumkatisha tamaa Levina mpaka akaona kuwa maisha yake hayana maana tena.

Zaidi ya hayo utu wake ulikuwa umedhalilishwa na jitihada za Saloti za kutaka kumbaka [Maana katika jamii ya Kitanzania inaaminika kuwa mwanamke akibakwa amependa mwenyewe.

Kutokana na Punch kuwalazimisha marafiki wa Levina wamtenge, kumdhihaki mbele ya kadamnasi, kumdhalilisha na kumuonea, kutokana na malalamiko yake kutoshughulikiwa na MUWATA kwa kumwambia kuwa hakuna awezaye kushindana na Punch, wakati wengine walikuwa wakimcheka tuu anavyolalamika na rafiki zake wakimuepuka, yote haya yamemfanya alazimike kukata maisha yake kwani aliamini jamii nzima ilitoa hukumu dhidi yake.

Punch ilifanikiwa kuondoa umoja kati ya wanawake. Saloti alifanikiwa kumkosanisha Levina na Modesta, mtu pekee ambaye ndiye alikuwa akimwamini, kwa kudai kuwa yeye ndiye alimpa ufunguo.

Ukweli ni kwamba funguo zote za Hall 7 [alimokuwa akiishi Levina] ziliweza kufungua angalau milango mitano, wakati katika Hall 3 bweni lingine la wanawake ufunguo mmoja unafungua milango yote ya gorofa hiyo.

Walimfuatafuata na kumgongea mlango usiku wa manane, walimtupia maneno machafu na kumtishia mlangoni pake, walifanya aonekane kama ‘mwenda wazimu’ na asiyefaa.

HATUA ZA UONGOZI WA CHUO KIKUU

Katika toleo maalum la Sauti ya Siti kuhusu ukatili wa kijinsia lililochapishwa mnamo Novemba 1992, Chemi Che-Mponda alisimulia namna ambavyo TAMWA iliendesha kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa kufanya mkutano wa dharura na wanafunzi wanawake, wahadhiri, wafanyakazi na wakazi wengine wa vyuo vikuu mnamo Februari 9, 1990.

Katika mkutano huo walitangaza kuwa jumuiya nzima ya Chuo Kikuu ilihusika katika kifo cha Levina, na wakashutumu utawala kwa kutochukua hatua ipasavyo za kuadhibu katika kesi za unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji chuoni hapo.

Walitoa wito kwa Chuo Kikuu kuwasimamisha chuo Victor na Sarota na kusambaratisha PUNCH.
Pia walitaka maafisa ambao walizembea kujibu malalamiko ya Levina wajiuzulu nyadhifa zao.
Sarota alifukuzwa Chuo Kikuu mwaka wa 1990, lakini akaruhusiwa kurudi mwaka wa 1991.
Licha ya ghasia miongoni mwa makundi ya wanawake, PUNCH iliendelea hadi mwishoni mwa miaka ya 1990, ilipopigwa marufuku kwa kuchapisha nyenzo za kumdhalilisha Rais wa wakati huo Ali Hassan Mwinyi.

UNYANYASAJI WA KIJINSIA VYUONI

Mnamo Novemba 27, 2018, mhadhiri Vicensia Shule alizungumza kwa utata dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye Twitter akimuomba Hayati Rais John Magufuli aliyekuwa chuoni hapo kufungua maktaba mpya.

Alindika “Baba Magufuli umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuzindua maktaba ya kisasa. Unyanyasaji wa kijinsia unatokea kwa kasi ya kutisha pale UDSM. Natamani ungekubali mwaliko wangu wa kukutana nawe, lakini usalama wako ulinipuuza.
Kulingana na Twitter hiyo “uliibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu athari za ukatili wa kingono katika vyuo vya elimu ya juu nchini.”

Tatizo linaloendelea la unyanyasaji wa kijinsia katika elimu ya juu linaonyesha uharaka wa kumkumbuka Levina Mukasa, na kutii ombi lililoandikwa la wanawake waliokusanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Februari 9, 1990: “Levina asife bure.”

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk Rose Reuben anapozungumzia madhara ya ukatili wa kijinsia vyuoni hususani rushwa ya ngono anasema “Umma unapaswa kujua na kuzingatia ukweli kuwa, digrii bila rushwa ya ngono ni digrii yenye tija kwa jamii na taifa.”

Utafiti wa TAMWA na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) uliofanyika mwaka 2021 umegundua unyanyasaji wa kijinsia sio vyuoni tu hata kwenye maeneo mengine ya kazi ikiwemo vyumba vya habari.

Izingatiwe kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007, mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake anaomba au kutoa upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kigezo cha kutoa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria, atakuwa ametenda kosa chini ya kifungu hiki.

Adhabu ya mtu huyu ni faini isiyozidi Sh milioni tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zote kwa pamoja.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2020 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ulibainisha sababu tano kuu zinazochochea rushwa ya ngono vyuoni kuwa ni pamoja na ukosefu wa maadili na ushawishi wa watu wenye madaraka.

Nyingine ni mfumo dhaifu wa kushughulikia tatizo hilo, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki kwa waathirika pamoja na mamlaka ya utoaji alama za mitihani kuachwa chini ya walimu pakee.

Mkufunzi wa Masuala ya Mawasiliano ya Umma, Mary Kafyome, anasema kutokana na ukweli kuwa katika vyuo vikuu wahadhiri wana mamlaka makubwa kwenye alama na matokeo ya mitihani ya wanafunzi, kama mhadhiri si mwadilifu, anaweza kutumia mwanya huo kudhalilisha wanafunzi.

 

 

Habari Zifananazo

8 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button