“Miaka 61 ya Mapinduzi nchi ina maendeleo makubwa”

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, amebainisha kuwa katika miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar nchi imeshuhudia hatua kubwa ya maendeleo katika miundombinu mbalimbali ikiwemo elimu, afya, umeme, maji, barabara, teknolojia, madaraja na bandari.
Dk Mwinyi ameyasema hayo kwenye mahafali ya 10 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume(KIST), Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar leo Desemba 21 ambapo amesema katika miradi yote hiyo wahitimu wa Taasisi hii ni miongoni mwa wahandisi ambao waliotoa mchango mkubwa sana kufanikisha maendeleo hayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Aidha, amewasisitiza wahitimu wa Taasisi  hiyo kuitafsiri elimu waliyoipata kwa vitendo badala ya nadharia ili kutoa mchango wao kwa maendeleo ya nchi.

SOMA: Mwinyi: Yajayo Zanzibar yanafurahisha

Rais Dk Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutambua umuhimu wa taasisi hiyo kama chachu ya maendeleo kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta mbalimbali.
Halikadhalika amesema kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni jitihada ya kutafsiri kwa vitendo dhamira ya elimu ya amali na ufundi na kuwapa mbinu wananchi za kujitegemea ikiwa ni hatua muhimu ya ilani ya Chama cha Afro Shirazi iliyokuwa na dira na malengo ya muda mrefu ya kuandaa rasilimali watu kwa ajili ya kuitumikia nchi na kusukuma mbele maendeleo.
Amesema hatua hiyo inakwenda sawasawa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 – 2025 inayoweka mkazo kwa vijana kupewa elimu ya amali na ufundi ili wajitegemee badala ya kusubiri ajira chache zilizoko katika mfumo wa Serikali.
Rais Dk Mwinyi ameeleza kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Nane, Serikali imeipatia taasisi hiyo, miradi mikubwa miwili ikiwemo kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika katika Sekta ya Uchumi wa Buluu pamoja na mafunzo katika sekta ya ufundi, sayansi na teknolojia yenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa ambayo kumalizika kwake kutaimarisha miundombinu ya Taasisi hiyo pamoja na rasilimali watu.
Advertisement