Mwinyi: Yajayo Zanzibar yanafurahisha

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa zaidi ya ilivyoahidi na kuwafananisha wale wanaojifanya hawaoni maendeleo hayo watayaona zaidi.

Ameyasema hayo alipozungumza na wananchi wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya juu ya kwanza visiwani humo, iliyopo eneo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Advertisement

Ujenzi wa Barabara hiyo ya juu ulianza Desemba Mosi, mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Machi 20 mwakani kwa gharama ya Dola za Marekani 19,010,501 (Sh 46,765,832,460).

SOMA: Rais Mwinyi: Zanzibar ni salama

Rais Mwinyi amesema amefurahi kuona kwa mara ya kwanza Zanzibar inapata barabra ya juu na kuongeza kuwa hiyo kwake ndiyo maana halisi ya uongozi wenye kuacha alama.

“Pale ninaposema tuwe viongozi wenye kuacha alama, namaanisha haya, hii ni alama ya kudumu, tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuyafanya haya na mengine ambayo tuliwaahidi wananchi,” amesema.

Ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kazi kubwa waliyofanya iliyosaidia kuvuka utekelezaji wa malengo ya ilani na kusema kuwa yale yaliyoahidiwa yameshavukwa kwa kiasi kikubwa na kuongeza kuwa kwa sasa serikali inatekeleza mambo ambayo wala hayapo kwenye ilani na kwamba wako kwenye hatua za mbele sana.

“Kuna wale ambao kazi yao ni kutupa majina, sasa leo (jana) naona watakuwa wamepata jina jipya hapa, maana tushatoka kwenye usemi wa bati sasa tuko kwenye usemi ‘my Flyover’ (Barabara yangu ya juu), sasa nataka niwaambie wale ndugu zetu ambao wanajifanya hawaoni, nataka niwaambie kama hawaoni ya ardhini basi watazame angani watuambie hawaoni, maana ardhini tushamaliza sasa tunakwenda angani, na kwenyewe kama hamuoni basi huo utakuwa ujuha, hakuna lugha nyingne,” amesema.

Amewataka watambue kwamba kazi ya kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye miundombinu ya barabara ndiyo kwanza imeanza, kwa kuwa sasa serikali ina mpango wa kujenga mradi wa makutano wa barabara nne za juu.

Amesema anashangazwa kuona watu wenye akili timamu wakilalamika kwamba serikali imekuwa ikijenga vichochoro badala ya barabara na kuwataka Wazanzibari watambue kwamba serikali yao imewapangia mambo
mazuri yanayokuja.