SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika(CAF) limeandaa uzinduzi wa mashidano ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17, Girls Integrated Football Tournament (GIFT) mwezi ujao yenye lengo la kukuza maendeleo ya soka la wanawake barani Afrika.
Kwa mujibu wa CAF, mashindano hayo yatafanyika kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam yakizishirikisha timu nane kutoka uknda wa CECAFA kuanzia Januri 7 hadi 18, 2025.
Timu zitakazoshiriki ni JKT Queens na TDS Girls Academy za Tanzania, Aigle Noir ya Burundi, Bahir Dar Kenema ya Ethiopia, Kenya Academy of Sports ya Kenya, Boni Consilli Girls Vocational Team ya Uganda, City Lights Football Academy ya Sudan Kusini na Hilaad ya Somalia.
CAF imesema mashindano haya yanatatumika kuonesha wanasoka chipukizi wa kike, kujenga uwezo wa wachezaji na kukuza soka la wanawake ngazi za CECAFA na Bara la Afrika.
Michuano hiyo ni sehemu ya mkakati wa CAF kuongeza ushiriki wa wasichana kwenye soka barani Afrika, kuhamasisha nchi wanachama na klabu kuwekeza katika vilabu vya wasichana, ligi na timu za taifa za wasichana za U17 na kutoa fursa kwa wasichana kuhama kutoka soka ya shule hadi soka la ushindani.
Pamoja na michuano hiyo, kutakuwa na matukio kama tamasha la soka kwa wasichana, kliniki za michezo na kampeni za uhamasishaji wa afya zitakazofanywa kwa ushirikiano na Shirikisho la Vyama vya Soka Ulaya(UEFA).