MARA: MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na mnyororo wa thamani wa mazao kwa kutumia mifumo rasmi ya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko.
Mtambi alisema kuwa mifumo ya stakabadhi za ghala na minada ya kidijitali itawawezesha wakulima kupata bei za haki kwa mazao yao, hivyo kuwalinda dhidi ya dhuluma za bei na vipimo visivyo sahihi.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mazao ya choroko na dengu Mtambi aliunga mkono mwongozo wa kitaifa wa biashara ya mazao ulioasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, alieleza kuwa mifumo ya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko inalenga kuwapa wakulima fursa ya kuamua bei kwa kuzingatia thamani halisi ya mazao yao.
Mlola pia alibainisha kuwa COPRA imejipanga kuhakikisha uwazi na haki vinazingatiwa katika biashara ya mazao. Vibali vya kusafirisha mazao kama dengu, mbaazi, choroko, soya, na ufuta vitatolewa kwa wanunuzi waliosajiliwa na walionunua mazao kupitia mifumo iliyoidhinishwa na serikali.
Mkutano huo umelenga kuwahamasisha wakulima na wadau wa kilimo kushirikiana katika matumizi ya mifumo rasmi ya biashara ili kuongeza thamani ya mazao, kuhakikisha masoko yenye tija, na kuchangia maendeleo ya uchumi wa mkoa wa Mara.