Miico wajikita kutatua udumavu Momba

SONGWE: KUTOKANA na Wilaya ya Momba iliyopo mkoani Songwe kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu ambacho ni asilimia 31.9 licha ya kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula, kumelisukuma shirika lisilo la kiserikali la MIICO wakishirikiana na Farm Africa, T marc na SNV kupitia mradi wa NOURISH kuimalisha lishe bora na usalama wa chakula kujenga jamii iliyobora.
Akizungumza katika Maonesho ya Afya na Lishe kijiji cha Ikana Wilaya ya Momba, Meneja wa Mradi wa Nourish kutoka shirika la MIICO Frimina Kavishe amesema kutokana na tafiti kuonesha kuwa Momba ina watoto wengi chini ya miaka mitano wenye utapiamlo na udumavu wao wamejikita kutoa elimu kuhusu lishe bora, usalama wa chakula na kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu suala la malezi ya watoto.
Amesema kuwa wamegundua kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea kukithiri kwa udumavu katika jamii ya wananchi wa Momba kuwa ni pamoja kuuza mazao ya chakula baada ya kuvuna, kula chakula cha aina moja , malezi ya watoto kuachiwa kundi la wanawake pekee na ukosefu wa elimu namna ya kutumia makundi sita ya vyakula yenye virutubisho vya kutosha.
Kavishe anasema wakishirikiana na serikali ya Wilaya ya Momba wameanza kutoa elimu kuhusu lishe bora, umuhimu wa kuwa na chakula cha kutosha , usalama wa chakula kuwafundisha kulima mazao yenye virutubisho lakini yanayoendana na mabadiliko ya tabia ya nchi na elimu kuhusu mgawanyo wa majukumu ya malezi ya watoto.
Tayari tumewafikia wananchi 2460 waliopo kwenye viikundi ambapo wanaume ni 1476 na wanawake 984 , kwa upande wa kaya zenye wanawake wajawazito na wenye watoto chini ya miaka miwili tumezifikia kaya 656 ambazo tunazipatia elimu kila wiki kuhusu namna ya kutumia makundi sita ya vyakula yenye virutubisho kuepusha mtoto aliyepo tumboni na baada ya kuzaliwa kupata utapiamlo na udumavu,” amesema Frimina.
Naye mratibu wa Mradi wa Nourish kutoka shirika la T Marck Farida Shaban anasema kutokana na changamoto za udumavu na utapiamlo katika mikoa ya Songwe na Rukwa ambayo inazalisha sana mazao ya chakula wao pia wamejikita kubadili tabia ya jamii katika maeneo muhimu hasa katika masuala ya ulaji, uandaaji chakula, Malezi ya Watoto na utunzaji chakula.
” Tunajua mabadiliko ya tabia huchukua muda mrefu hivyo tumeanza kutoa elimu kuhusu umuhimu jamii kushiriki kwa pamoja katika majukumu ya kulea watoto hasa wazazi wakiume, kubadilili tabia ya kushiriki kwa pamoja katika masuala ya kutenga chakula na usalama wa chakula pamoja umuhimu wa kutumia makundi sita ya vyakula na namna ya kuviandaa” amesema Farida.
Kwa upande wake mwakilishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba Veronica Komanya amesema wakishirikiana na wadau mbalimbali wa lishe wanamatumaini makubwa ya udumavu kupungua kutokana wananchi wengi kuanza kubadilika baada ya kupata elimu ya lishe.
Amesema kupitia mradi huo matarajio makubwa ni kuonana jamii ya Momba inapata chakula cha kutosha, inapata lishe bora , kuzalisha mazao yanayoendana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja kuhakikisha wanabafulika na kutumia makundi sita ya vyakula vyenye lishe bora.
Amezitaja kata saba ambazo zimeanza kunufaika na mradi huo kuwa ni Ikana, Ndalambo, Miyunga, Chitete, Kapele, Nzoka na kata ya Musangano , ambapo tayari wananchi 2460 kupitia viikundi tayari wamepata elimu kuhusu lishe bora pamoja na usalama wa chakula , huku wanawake wajawazito na wenye watoto wachanga wakipatiwa mafunzo namna ya kuwapatia lishe bora ili kuwaepusha watoto kupata udumavu na utapiamlo.
Kwa upande wake Jolina Siame ambaye ni diwani wa jata ya Ikana amesema mradi wa Nourish umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwani wameanza kutunza chakula ili kuwa na uhakika wa chakula , kulzalisha mazao yenye virutubisho yenye kuvumilia ukame wakishirikiana na watalaam wa kilimo ngazi ya kata pamoja na watalaam wa mradi kutoka shirika la Miico chini ya Mradi wa Nourish kupitia mashamba darasa .