MOROGORO: MIILI ya watu watano kati ya 15 waliofariki kutokana na ajali ya lori kugongana na basi dogo la abiria imetambuliwa hadi kufikia Desemba 18, 2024.
Mganga Mfadhiwi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu amesema hayo leo na kuongeza kuwa siku ya tukio hilo Desemba 17, 2024 hospitali ilipokea miili ya watu 14 waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo pamoja na majeruhi wanane.
Mganga mfadhiwi wa hospitali hiyo amesema kuwa kati ya miili iliyopokelewa siku ya tukio, nane ni wanaume na sita wanawake.
Dk Nkungu amesema wakati wakiendelea kuwapatia huduma majeruhi, mmoja ambaye ni mtoto wakike mwenye umri wa miaka minane alipoteza maisha akipatiwa matibabu na kuongeza idadi ya vifo kufikia 15.
Amesema hadi Desemba 18, 2024 miili mitano yote ya wanaume ilikuwa imetambuliwa na ndugu zao ambayo ni Rashid David Mtafya ambaye ni dereva wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Kisonda Ndaluma Mohiba ambaye ni mfanyabiashara na Juma Ally Hassan ambaye ni dereva basi dogo.
Mingine iliyotambuli ni Hamza Ally Digali ambaye ni mfanyabiashara na Mohomed Kollo Mkusa kwa jina maarufu Abdul Kolllo Mkusa ambaye ni dereva wa lori, wakati miili mingine 10 hawajatambuliwa na kati ya hiyo saba ni ya wanawake na mitatu ni ya wanaume.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa kuwa utaratibu wa kiserikali watakaa na hiyo miiili kwa muda wa siku 14 wakiwa wameihifadhi chumba cha maiti katika hospitali hiyo na ndugu wote ambao wanahisi ndugu zao walikuwepo kwenye hiyo basi dogo na labda mauti yamewakuta matangazo yametokewa kwa kutoa namba ya simu ya hospitali
“ Tunawakaribisha kuja kuwatambua ndugu zao na siku zikupita serikali itafanya utaratibu wake wakuhifadhi miili hiyo ( Kuizika) kama hakuna mashauri yanayohusika kimahakama,” amesema Dk Nkungu.
Amesema majeruhi mmoja alikuwa akipatiwa huduma katika Kituo cha Afya Fulwe Mikese na kufanya idadi ya majeruhi kuwa nane, na hadi sasa Hospitali ina majeruhi saba waliolazwa na kati yao watano ni wanaume na wawili ni wanawake .
“ Leo nimepita mweneywe kuwaona na wote hawajambo na wanaendelea vizuri na wanamaumivu madogo madogo na mivujiko na wanashughulikiwa na Madaktari bingwa wa mifupa,”amesema Dk Nkungu.