Mikindani watakiwa kujitokeza mafunzo ufundi stadi

RAI imetolewa kwa vijana katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, wajitokeze kwa wingi kwenye mafunzo yatayotolewa bure kwa vijana 50 wa manispaa hiyo kuhusu kuimarisha sanaa, utamaduni pamoja na ufundi stadi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program hiyo ya kuimarisha sanaa, utamaduni na ufundi stadi kwa vijana hao, Ofisa Utamaduni Mkoa wa Mtwara Fatuma Mtanda amesema fursa hiyo ni muhimu ambayo inapaswa kuchangamkiwa na vijana hivyo washawishike na wajitokeze kwa wingi katika mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yanatolewa na Shirika lisilo la kiserikali linalojishughuli na masuala ya sanaa,utamaduni mkoani mtwara (ADEA) kwa udhamaini wa Shirika lisilo la kiserikali linalojishulisha na masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani la UNESCO, lengo ni kuwaongezea vijana hao elimu na ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi mbalimbali na kukuza uchumi wao.

Advertisement

‘’Niwaombe sana vijana pmaoja na wazazi mtakaposikia tangazo hili, tuwe tayari kuwashawishi vijana wetu na vijana wenyewe washawishike na kwenda kuchukua fomu na kujaza na kujiunga na mafunzo haya ambayo yatawasaidia sana kukuza elimu na ujuzi utakawasaidia kufanya kazi mbalimbali na kujiongezea kipato katika maisha’’alisema Mtanda

Hata hivyo amewaomba vijana hao watakaoshiriki mafunzo hayo kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ya kutosha wakati wa mafunzo na baada ya mafunzo kipindi watakapotumia ujuzi huo katika shughuli zao mbalimbali na kufanya hivyo itasaidia kuwavutaia wateja katika kazi hizo.

Mkurugenzi wa Shirika hilo la ADEA, Saidi Chilumba amesema mafunzo hayo maalumu yatatolewa katika fani nne za mikono ikiwemo uchoraji, uchongaji, ufundi selemala pamoja na ufundi chuma na vijana wanaohitajika ni wale ambao angalu wanamekuwa na uzoefu katika fani hizo ili waweze kuongezewa chachu ya ubunifu wao.

Amesema sababu kubwa iliyopelekea kuandaa mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na wengi wao kujisahau kuwa kuna maisha baada ya ujana na wengine wakijikita kwenye fursa za bodaboda fani ambayo siyo endelevu kwa maisha ya baadae kwahiyo wanataka wawapatie vijana fursa ya ujuzi ambapo vijana wanaotakiwa kushiriki mafunzo ni kuanzia umri wa miaka 18 mpaka 35.

Kaimu Mratibu wa Mafunzo kwa vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Mashiriki inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara, Elias Nzunda amewataka vijana hao kuchangamkia fursa ya kupata mafunzo hayo na wao kama VETA watashirikiana kikamilifu na ADEA kuhakikisha kile wanachopaswa kukipata kinapatikana.

Kwa upande wao baadhi ya vijana hao akiwemo Ally Selemani Mkazi wa Kijiji cha Ruvula Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ‘’Hii fursa ni mzuri sana na kama tutakuwa na mwamko sisi vijana baada ya miezi kadhaa tutakuwa na mafanikio makubwa sana kwasababu hiyo ni fani na fani haizeeki’’