Mikopo yawainua wenye ulemavu Iringa

IRINGA: Mikopo inayotolewa na Serikali kwa watu wenye ulemavu imeanza kubadili maisha ya baadhi ya wanufaika mkoani Iringa, huku baadhi yao wakifanikiwa kuanzisha biashara, kuongeza kipato na kutoa ajira kwa wengine.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, alipofanya ziara mkoani Iringa kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa programu za uwezeshaji watu wenye ulemavu.
Nderiananga amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kupata mikopo na fursa nyingine za kiuchumi, akiwataka kuzitumia kujikwamua na kujenga maisha ya kujitegemea.
“Mkopo huu si hisani. Ni fursa ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kujitegemea, kuongeza kipato na hata kuajiri wengine,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa iliyotolewa na mratibu wake wa mikopo, Sunday Mathayo tangu kurejeshwa kwa mpango wa mikopo mwaka 2024, Manispaa hiyo imetoa Sh bilioni 2.14 kwa vikundi 183 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kati ya fedha hizo, vikundi 27 vya watu wenye ulemavu vimepatiwa Sh milioni 189.76, huku jumla ya watu 951 wakinufaika na mikopo hiyo kwa makundi yote.
Nderiananga amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kuangalia fursa zaidi ya mikopo, ikiwemo kushiriki katika zabuni za Serikali na kuzalisha bidhaa na huduma kama matofali, sare za shule, nishati safi na bidhaa nyingine zinazohitajika katika jamii.
Amesema kumuwezesha mtu mwenye ulemavu kiuchumi kunaweza kusaidia kuajiri watu wengine na hivyo kuchangia maendeleo ya jamii.
Aidha, ameitaka Iringa kuongeza kasi ya kuwawezesha watu wenye ulemavu, akisema kiwango cha mikopo wanachopata mkoani humo kinapaswa kuongezeka kulingana na mahitaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Iringa, Shabani Shomari, amesema elimu zaidi inahitajika ili kuhakikisha mikopo inayotolewa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Amesema baadhi ya watu wenye ulemavu wamekuwa wakichukua mikopo lakini fedha hizo zinaendeshwa na ndugu au watu wengine, hali inayoweza kusababisha kushindwa kurejesha mikopo.
“Tunawahitaji watu wenye ulemavu wapewe elimu ya kutosha kuhusu mikopo hii ili waielewe na kuitumia kwa shughuli zao zilizokusudiwa,” amesema.

Nderiananga pia amesisitiza umuhimu wa kupambana na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu, akiwataka walengwa kujiamini na kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri na wadau kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata elimu, mitaji na fursa za masoko ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.



