Mil 584/- kukamilisha shule wilaya ya Chato

SERIKALI imepanga kutumia sh milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Butengolumasa wilayani Chato mkoa wa Geita ili kusogeza huduma ya elimu.

Mradi wa ujenzi wa shule ya Butengolumasa ulianza mwaka Oktoba 10, 2024 chini ya mkandarasi wa kampuni ya Nekateck Construction Company Limited.

Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Mbezi Rugakila ametoa taarifa ya mradi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita alipozuru Kijiji cha Butengorumasa kukagua mradi huo.

SOMA: Serikali kuijenga Chato hadhi ya mkoa

Rugakila amesema kati ya pesa hizo, sh milioni 77 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, sh milioni 209 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa pamoja na ofisi moja.

“Pia kuna ujenzi wa majengo ya maabara tatu za biolojia, kemia na fizikia kwa sh milioni 153, jengo la Tehama sh milioni 51 na matundu manne ya vyoo vya wavulana kwa sh milioni 10.

“Matundu manne ya vyoo vya wasichana na chumba maalum kwa sh milioni 12, maktaba moja kwa sh milioni 61, kichomea taka kwa sh milioni 4 na tenki la maji sh milioni 3.9.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombat amesema ujenzi wa shule umetumia mkandarasi ili kuhakikisha ubora wa majengo unaakisi thamani ya pesa iliyotolewa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kufanikisha sera ya elimu bila malipo inatekelezwa pasipo kuwa na changamoto ya miundombinu.

Amesema kila mwezi mkoa huo  unapokea takribani sh bilioni 1.2 kama sehemu ya kufanikisha sera ya elimu bila malipo huku usimamizi thabiti unafanyika kufanikisha malengo.

Shigela ameagiza mchakato wa kuisajili shule hiyo mpya ukamilishwe kwa haraka ili mwaka mpya wa masomo 2026 unapoanza, wanafunzi wapate nafasi ya kuanza masomo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button