SERIKALI imeweka wazi kuwa inaendelea kuboresha miundombinu na huduma za kijamii inayotosheleza mahitaji ya wànanchi kabla ya kuitizama upaya ajenda iliyokuwepo ya Chato kuwa mkoa.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema hayo akiwa kijiji cha Igando kata ya Bwele wilayani Chato katika ziara maalum ya mawaziri inayofanyika nchi nzima kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali.
Mavunde amesema kila kitu kinaendelea kutekelezwa kwa kasi na ubora wake ndani muda na hivo wananchi wa Chato wanapaswa kuwa na amani na imani na serikali yao kwani ombi la Chato kuwa mkoa halijasaulika.
“Rais anayo dhamira ya dhati, tunataka kuendelea kuijenga Chato, Chato iendelee kuimarika, lakini mheshimiwa Rais kufikia huko lazima kwanza kuna kazi ifanyike.
“Kazi yenyewe ndio hii tunaifanya, lazima tuweke huduma sawa za wananchi, tuijenge vizuri tufikie katika dhamira kama hiyo ili tuchukue hatua ya kufikia huko.
“Ndio maana mheshimiwa Rais ameagiza nguvu kubwa iletwe katika Wilaya ya Chato, kuijenga Chato kwa kuwa hakuna kilichosahaulika,” amesema Mavunde.
SOMA: JKCI, hospitali ya rufaa Chato kutibu moyo kisasa
Amesema katika kufanikisha hilo ndani ya miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita wilaya ya Chato imepatiwa Sh bilioni 109 kati ya takribani Sh bilioni 800 ambazo mkoa wa Geita umepatiwa kutekeleza shughuli za maendeleo.
Awali Mavunde ameweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya lami yenye umbali wa kilomita moja iliyopo kituo cha mabasi cha Ihumwa na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa madarasa shule ya sekondari Makurugusi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema mkoa umeendelea kufunguka kwani kati ya vijiji 486, tayari vijiji 483 vimeshafikiwa na umeme huku vikiwa vimesalia vijiji vitatu pekee vilivyopo kisiwani Kata ya Izumacheli.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chato, Christian Manunga ameiomba serikali kuendelea kujenga barabara ili kuziunganisha kata zote ndani ya halmashauri hiyo kuendelea kuifungua wilaya hiyo.