TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imeanza kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia mashine za kisasa. Mashine hizo zina uwezo wa kugundua magonjwa ya moyo kwa usahihi wa asilimia 95.
Huduma hizi zinatolewa wakati wa maonesho ya 7 ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili, mjini Geita.
Daktari bingwa wa moyo kutoka JKCI, Dk Salehe Mwinchete amesema huduma hizo zinafanyika katika mikoa ya pembezoni mwa Tanzania ili kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa.
Tanzania ikiwa nchi iliyopewa jukumu la kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, inahakikisha inafikia wananchi wengi zaidi, hususan wale walioko mikoani.
Dk Liberius Libent kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato amebainisha kuwa ushirikiano kati ya JKCI na CZRRH ulianza mwaka 2022 kwa lengo la kuikuza hospitali hiyo na kuiwezesha kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa ufanisi zaidi.
SOMA: JKCI, hospitali ya rufaa Chato kutibu moyo kisasa
Amesema kupitia ushirikiano huo, hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za upasuaji wa mishipa ya damu na hadi sasa wagonjwa wanne wamefanyiwa upasuaji huo kwa mafanikio.
Akizungumza baada ya kupatiwa huduma, Robert Nangu mmoja wa wananchi waliopimwa afya zao kwenye banda la JKCI, alitoa pongezi kwa JKCI na CZRRH kwa kuwasogezea huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Amesema huduma hizo ni muhimu kwani magonjwa ya moyo yamekuwa chanzo kikuu cha vifo kwa Watanzania wengi ambao mara nyingi hawana fursa ya kugundua maradhi hayo mapema.
“Watanzania wengi tunasumbuliwa na maradhi ya moyo ambayo mara nyingi hupelekea vifo bila kujua, tukipata nafasi kama hii ya kufikiwa na huduma hizi tusijiulize mara mbili, tujitokeze kupima afya zetu,” amesema Robert.
Huduma hizi zinaendelea kutolewa kwa wananchi wote wanaotembelea maonesho hayo, lengo likiwa ni kuboresha afya za Watanzania na kuokoa maisha kwa kugundua magonjwa ya moyo mapema.
Comments are closed.