Uhusiano Tanzania, China, lulu maendeleo, ubora JKCI

KUNA msemo mmoja wa kale wa Kichina wenye kuelezea manufaa ya ushirikiano, ambao kwa lugha ya Kichina anatamkwa ‘Gū zhǎng nán míng,’ ambapo tafsiri yake kwa Kiswahili ni kuwa ‘Huwezi kupiga makofi kwa mkono mmoja pekee.’

Nathubutu kusema huu ni moja kati ya misemo dhabiti sana!

Niulize, kwa nini? msemo huu unasisitiza umuhimu wa ushirikiano katika maendeleo na motisha katika kufikia mafanikio kwa njia ya ushirikiano.

Tunaweza kuufananisha pia na msemo maarufu wa Kiswahili, ‘kidole kimoja hakivunji chawa’ ama sawia na hisia zinazoonyeshwa katika msemo maarufu wa Kiingereza unaotokana na wimbo wa “It Takes Two to Tango” ulioandikwa na Al Hoffman na Dick Manning mwaka wa 1952.

Hivi karibuni katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji, Dkt Peter Kisenge, alisisitiza umuhimu wa msemo huo wakati wa hafla ya muendelezo kutambua umuhimu wa uhusiano mkubwa kati ya Tanzania na China.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya JKCI yanatokana na mchango makubwa sana na uhusiano thabiti kati ya nchi hizi mbili, hasa akasisitiza jukumu kubwa lililofanywa na China kwa kutoa ufadhili wa awali wa jumla ya 16bn/- kwa ajili ya ujenzi wa taasisi hiyo.

Dk Kisenge aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na waandishi wa habari wakati wa Mahojiano ya maalumu yaliyopewa jina ‘Mahojiano ya Pamoja kati ya China na Afrika katika Enzi Mpya’ ikihusisha waandishi wa ‘People’s Daily’ ya China na waandishi kutoka vyombo vya Habari vya Tanzania’ yaliyofanyika katika taasisisi hiyo jijini Dar es Salaam.

“JKCI ni matokeo ya uhusiano baina ya Tanzania na China, na kituo hiki kilikuja baada ya mkutano muhimu wa aliyekuwa Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Hou Jing Tao mwaka 2006 na kukubaliana kujenga kituo hiki,” alisema.

SOMA: Watoto 500 kufanyiwa upasuaji JKCI

Akielezea zaidi, Dk Kisenge alifafanua juu ya msingi wa kihistoria wa ushirikiano kati ya Tanzania na China, tangu enzi za viongozi waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Abeid Amani Karume kwa Tanzania pampja na Mao Zedong, Zhou Enlai, na baadaye Kiongozi Mkuu Deng Xiaoping kwa upande wa China.
Alisema uhusiano wa kudumu baina ya nchi hizi mbili ulioanzishwa mwaka 1964 unazidi kushamiri hadi sasa chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping wa China na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Katika mahojiano hayo, Dk Kisenge pia alibainisha kuwa uanzishwaji wa JKCI uliwezekana kwa ufadhili mkubwa wa serikali ya Tanzania na China, na kuifanya kuwa moja ya mafanikio ya uhusiano wa Tanzania na China. Serikali ya China ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kujenga jengo la JKCI ambalo awali lilikuwa na vitanda 152 lakini kwa sasa lina vitanda 252.

Aliongeza kuwa ufadhili wa vifaa mbalimbali vya matibabu vinavyotumika katika upasuaji na matibabu ya moyo katika taasisi hiyo pia ulitolewa na serikali ya China.

“Sambamba na hayo, pia tumekuwa tukipokea madaktari wengi kutoka China, ambapo JKCI mpaka sasa tumepokea jumla ya madaktari 11 ambao wote wanakuja kwa programu maalumu ya miaka miwili ya kufundisha madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na afua zake,” alifafanua.

Aliongeza kuwa kwa sasa JKCI imeajiri madaktari bingwa kabisa wa magonjwa ya moyo zaidi ya 14, wakiwemo madaktari bingwa watatu kutoka China, kati ya watatu hao mmoja ni daktari bingwa wa wagonjwa mahututi, mwingine ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, na wa tatu ni bingwa wa upasuaji wa moyo.

SOMA: JKCI kutoa huduma bure Namtumbo

Kwa mujibu wake ni kwamba, baadhi ya madaktari wa Tanzania katika taasisi hiyo wamepata mafunzo yao ndani ya nchi, huku wengi wao wakipata mafunzo yao nje ya nchi, nchini China, Marekani na kwingineko.

Aidha, alibainisha kuwa, ushirikiano wa China na Tanzania umezaa matunda mengi hadi sasa, na JKCI sasa ni moja ya taasisi za juu za elimu ya kielektroniki/ ‘electrophysiology institutes’ katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Hadi hivi sasa, JKCI ni miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa matibabu ya moyo na waanzilishi Afrika Mashariki na Kati linapokuja suala la kutoa huduma bora za moyo na upasuaji,” alisisitiza Dk Kisenge.

Sanjari na hilo, alisema kuwa kwa sasa JKCI ndiyo hospitali inayohudumia wagonjwa wengi zaidi kati ya hospitali zote za Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa inaweza kufanya upasuaji wa moyo zaidi ya wagonjwa 700 kila mwaka.
Akifafanua zaidi alieleza kuwa JKCI inatibu zaidi ya wagonjwa 3000 katika maabara yake kubwa ya katheta (Cath lab) kwa watu wazima na watoto, ambapo Tanzania ndiyo nchi pekee katika Afrika Mashariki na Kati—inawezekana hata Afrika—inayoweza kutibu wagonjwa kwa kiwango hiki, ikizidiwa kwa uchache na baadhi ya nchi za Afrika Kaskazini na nchi ya Afrika Kusini.

“Na haya ni matokeo chanya kutokana na msaada wa serikali ya China kwa serikali ya Tanzania katika kuanzisha JKCI, ambayo sasa ni hospitali kubwa zaidi barani Afrika inayotoa huduma za upasuaji wa kipekee wa moyo na afua,” alisisitiza.

Taasisi hiyo sio tu imestawi katika kutoa huduma maalum za moyo lakini pia imeibuka kuwa kitovu cha mafunzo ya matibabu na kubadilishana maarifa.

Alisema kupitia ushirikiano huo, wataalam kutoka China kama vile Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Dkt Zhao Lijian, JKCI imeongeza uwezo wake katika kutibu magonjwa magumu ya moyo na mishipa, na kutoa taratibu za kisasa ambazo hazikuwa zikipatikana nchini hapo awali.

Akitoa maelezo yake ya muda aliotumia kufanya kazi JKCI, Dk Zhao alitaja kuwa hiyo ni ziara yake ya pili katika taasisi hiyo.
Akiwa amepewa jina la Dkt ‘JO’ kutokana na watu wengi kupata ugumu kutamka jina lake la Dk Zhao, alieleza jinsi anavyofurahia kazi yake nchini Tanzania.

“Ninapenda kufanya kazi hapa; napenda kufanya kazi na madaktari wa hapa na kuwafundisha jinsi ya kufanya taratibu sahihi kwa matibabu ya watoto,” alibainisha.

Aidha alibainisha kuwa katika miaka yake miwili ya awali akiwa JKCI miaka mitano iliyopita, idadi kubwa ya madaktari wazawa walikosa utaalamu thabiti kufanya taratibu za matibabu ya watoto. Hivyo, kufuatia ushirikiano, madaktari wengi wa ndani wamepata utaalamu huo.

“Nilijenga mahusiano mazuri na wenzangu (madaktari wazawa), hata nawaaga madaktari wengi akiwemo Profesa Mohamed Janabi (ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) waliniomba niongezewe muda, hivyo nikiwa China, Nilikumbuka sana JKCI, kwa hivyo nilituma maombi ya muhula mwingine wa miaka miwili,” alisema huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.”Ndio maana niko hapa tena na nitapenda kurudi hapa tena na tena,” aliongeza.

Kwa upande wake, Daktari wa magonjwa ya moyo kwa watoto Dk Megha Unadkat, alisema kuwa kufanya kazi na wataalam wa magonjwa ya moyo wa China kumethibitika kuwa na manufaa sana kwani wanasaidiana katika kubadilishana uzoefu na kurahisisha kazi.

Alisema kutokana na umahili wa lugha wa Dk Zhao, akiwa na uwezo wa kuzungumza Kiingereza fasaha na Kiswahili kiasi, hivyo hakuna tatizo kabisa katika mawasiliano.

“Hakuna hata kikwazo kidogo cha lugha kwa sababu Dk Zhao anazungumza kidogo Kiswahili na Kiingereza kizuri sana,” alisema Dk Megha.

Naye, Dk Angela Muhozya, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI, alisisitiza umuhimu wa muunganiko huo akisema kupitia juhudi hizi za ushirikiano, kuwezesha kubadilishana utaalamu na kukuza mazingira mazuri ya kujifunza kwa madaktari wazawa, Alisisitiza umuhimu wa madaktari wazawa  kuimarisha ushirikiano huu na kuendelea kukuza uhusiano kati ya Tanzania na China kwa manufaa ya pande zote za maendeleo ya huduma za afya katika eneo hilo.

Ujumbe wa waandishi kutoka ‘People’s Daily’ ya China hivi sasa ulikuwepo nchini kwa ziara ya kutembelea miradi ya ushirikiano kati ya China na Afrika katika mradi wa walioupa jina ‘enzi mpya’.

Gazeti la People’s Daily ni gazeti rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na ndilo gazeti lenye ushawishi na mamlaka zaidi nchini China kuwakilisha sauti ya serikali kuu ya China.

Itakumbukwa kuwa, Januari mwaka jana, serikali za Tanzania na China pia zilitiliana saini makubaliano ya kufanya upembuzi yakinifu wa kupanua taasisi ya JKCI kwa kujenga kituo cha magonjwa ya moyo kilichopo Mloganzila jijini Dar es Salaam.

Upembuzi yakinifu ulifanyika kwa muda wa miezi mitatu kabla ya ujenzi kuanza mapema mwaka huu, na mradi utachukua miaka miwili kukamilika.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu, alisema lengo la kituo hicho itrakua ni kuifanya JKCI kuwa kituo bora cha magonjwa ya moyo na mishipa Afrika Mashariki na Kati.

“Naipongeza Serikali ya China kwa kuendelea kudumisha mahusiano mazuri na sisi, na tumekubali kuanza kufanya upembuzi yakinifu ili kuboresha JKCI ili iweze kukua zaidi.

“Kwa sasa JKCI inahudumia wagonjwa wengi ndani na nje ya nchi na inatoa huduma za matibabu ya moyo Afrika Mashariki na Kati; hivyo basi, wazo la kupanua kituo hiki ni kuleta unafuu kutokana na ongezeko la wagonjwa,” alisema Prof Nagu.

Habari Zifananazo

Back to top button