HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imetenga Sh milioni 827 kwa ajili ya mikopo ya asilimia10 kwa wananchi walio kwenye vikundi vya ujasiriamali vya vijana, wanawake na wenye ulemavu ili waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Malmashauri Manispaa hiyo, Emmanuel Mkongo amesema hayo wakati wa kuhitimishwa mbio za pole zilizoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ambazo zililenga kuhamasisha masuala ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mkongo amesema kuanzia Oktoba 3, mwaka huu taarifa imetolewa kwa wananchi ya kuanza utaratibu mpya wa utoaji mikopo ya makundi ya wanawake,vijana na wenye ulemavu .
“Tumeshaanza rasmi kwa makundi haya na sasa yajitokeze kuomba mikopo hii hadi kufikia Oktoba 15, mwaka huu,” amesema Mkongo.
Mkongo amesema mikopo hiyo kulingana na maelekezo maapya inaombwa kwenye mfumo rasmi ambao ulishaandaliwa , na kwamba vikundi vinapaswa kujiandikisha kwenye maeneo yao ya kata husika.
“Mikopo inachakatwa na yale maandiko, na miradi yao inafanyiwa uchambuzi na wakati mwingine Maofisa Maendeleo ya Jamii wa zile kamati za mikopo watatembelea na kujiridhisha na hiyo miradi “ amesema Mkongo.
Mkongo amesema kuanzia Oktoba hadi Novemba mwaka huu , manispaa inatarajia kuchakata na kutoa fedha kwa zaidi ya Sh milioni 800.
“ Kitu cha msingi ni wale wenye sifa kuomba kwenye mfumo na wakishaomba utaratibu utafanyika ,na wale wenye kupata changamoto ya kutumia mifumo tunawashauri wafike maeneo yao ya kata ama kwenye Ofisi kuu ya halmashauri ili wapate msaada” amesema Mkongo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala alisema serikali imeboresha upatikanaji na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 baada ya kusitiwa kwa sababu mahususi kutokana na kwamba wale waliokuwa na sifa walikuwa hawapati mikopo hiyo.
Kilakala amesema kulikuwepo na baadhi ya watumishi walituhumiwa kutengeneza vikundi hewa ambavyo haviwanufaishi wananchi .