‘Mila ya kuwekeza mke tumboni ina madhara’

SERIKALI imesema mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kihisia, ndoa za utotoni na inamnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika.

Kauli hiyo imetolewa na Wazirio wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi, Dk Dorothy Gwajima alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mary Azan Mwinyi aliyehoji serikali ina mpango gani wa kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama hasa mikoa ya Manyara na Arusha.

“Serikali inatambua kuwa kuna mila zenye faida ambazo zinapaswa kuendelezwa na mila zenye kuleta madhara ambazo Mhe. Mbunge ameziita “Mila potofu”, ikiwemo mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama.

“Mila hii ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kihisia, ndoa za utotoni na ina mnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika.

“Mheshimiwa Spika, katika kutokomeza mila za aina hiyo, serikali imeandaa utaratibu wa kuendesha majadiliano kwa kuwa masuala ya kimila yanahitaji umakini mkubwa katika kuyajadili.

“Wizara imeandaa mwongozo wa kuendesha majadiliano unaojulikana kama “Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji Majadiliano Kuhusiana na Mila na Desturi zenye Madhara kwa Jamii wa mwaka 2022”.

“Majadiliano hayo yanakuwa ni jumuishi yanayohusisha viongozi wa mila, viongozi wa dini, wazee maarufu na wataalamu waliopo katika ngazi ya jamii, ili kuja na ujumbe mahsusi wenye lengo la kutokomeza mila zenye madhara ikiwa pamoja na kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama,” amesema Waziri Gwajima na kuongeza kuwa:

“Natoa wito kwa wataalamu wa maendeleo na ustawi wa jamii waliopo ngazi za jamii kuandaa majukwaa ya kuongoza majadiliano kuhusu mila hiyo yenye madhara ya kuwekeza mke akiwa tumboni na kuja na jumbe mahsusi, ili kutumika kwenye majukwaa tofauti, kutoa elimu ikiwa pamoja na nyumba za ibada.

“Aidha, kupitia radio za kijamii zilizopo Mikoa ya Manyara na Arusha; jumbe hizo zitawanywe ili kuendelea kuelimisha jamii,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button