Wazazi watakiwa kulea watoto kwenye maadili mazuri

MTWARA: Wazazi na walezi mkoani Mtwara wameshauriwa kulea watoto katika maadili mazuri kuanzia mavazi, lugha ya kuongea na namna ya kuishi na watu, ili kuwa na kizazi bora chenye nidhamu katika jamii.
Hayo yameelezwa wakati wa mahafali ya Shule ya Msingi na Awali ya East Gate iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Wakizungumza katika maafali hayo, baadhi ya wazazi akiwemo Joyce Desmund, amesema wazazi wanapaswa kufatilia tabia na mienendo ya watoto wao ili kuwafahamu mazingira yao badala ya kutumia muda mwingi kwenye harakati za maisha pekee.

‘’Niwaombe wazazi wenzangu tutenge muda wa kuhakikisha tunawafatilia watoto wetu ili kujua tabia na mienendo yao, lakini unakuta muda mwingi sisi tuko tu bize na harakati au majukumu ya maisha kwa hali hii unakuta watoto wanakuwa huru,’’amesema Joyce
Mzazi mwingine Luyce Majaliwa amesema serikali siyo ya kulaumiwa kwa malezi ya watoto kwa kuwa malezi yanaanzia nyumbani kwa baba na mama, hivyo wazazi wote wawili ndio msingi mkubwa wa malezi bora kwa watoto.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ambaye ni Ofisa Elimu na Utawala wa Shirika lisilo la kiserikali mkoani humo la EdUKaid, Emmanuel Sanga ametoa wito kwa wazazi kujenga utamaduni wa kuwasimamia na kuwafatilia watoto katika ratiba za nyumbani.



