MKOA wa Geita umefanikiwa kupunguza mimba za utotoni kwa takribani asilimia 40 kutoka mimba 20 kwa kipindi cha Januari hadi Agosti 2023 mpaka mimba 12 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2024.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo ametoa taarifa hiyo atika uzinduzi wa Kampeni ya Tuwaambie Kabla hawajaharibika iliyofanyika mjini Geita.
Amesema hayo ni matokeo ya elimu inayoendelea kutolewa ingawa mimba za utotoni bado ni janga la kitaifa ambapo kila mmoja akishiriki kwenye kampeni ya Tuwaambie Kabla Hawajaharibika itawezekana kumaliza tatizo.
Kamanda amebainisha kuwa pia matukio ya mauaji yamepungua mkoani Geita kwa asilimia 37 kutoka matukio 89 kwa kipindi cha Januari hadi Agosti 2023 mpaka matukio 56 sawa na upungufu wa matukio 33,”
“Ila bado tuna changamoto matukio ya ubakaji, mwaka jana Januari mpaka Agosti 2023 tulikuwa na matukio 71 lakini kwa kipindi kama hicho mwaka huu tuna matukio 9, matukio haya yanaogofya sana kwa sababu mengine ni baba anabaka mtoto wake wa miaka mitatu, mtoto wa miaka sita ama saba, sijui ni imani za kishirikina, tamaa za kimwili au ni ibilisi kwa kweli ni changamoto,”
“Kupitia kampeni hii tutawaambia wamama, wasiwaamini kina baba ikibidi, ukimuona baba anamshika shika mtoto maziwa ogopa huyo baba inawezekana mganga kamwambia kabake mtoto wako,” amesema Kamanda.
SOMA: Jeshi la Polisi latakiwa kutunza maadili
Amesema matukio ya watoto kupotea yameongezeka kutoka matukio mawili kwa Januari hadi Agosti 2023 mpaka matukio saba yaliyoripotiwa kwa kipindi hicho mwaka 2024 ingawa wote walitafutwa na kupatikana.
“Tafadharini wazazi muwatunze watoto, asilimia kubwa ya watoto hawa walioibiwa uzembe mkubwa ni wa wazazi, sasa mzazi unatafuta pesa unasahau mtoto, hivo tunao wajibu wa kuwaangalia na kuwatunza watoto.
“Ni wakati gani tunawaambia hawa watoto kuhusu maisha yao ya baadaye, wajibu wetu ni nini kuhusu hawa watoto, kwa hiyo sisi wenyewe ni chanzo cha watoto kupotea,” amesema Kamanda Jongo.
SOMA: RPC Geita aonya unyanyasaji dhidi ya wanaume
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameagiza ushiriki wa taasisi na wazazi wote katika kampeni ya Tuwaambie Kabla Hawajaharibika ili izae matunda.