KOCHA Mkuu wa timu ya Geita Gold ya mjini Geita, Fred Felix Minziro amesema kiini kikubwa cha washambuliaji wazawa kutofanya vizuri ni kutokuwa na njaa ya mafanikio wanaposajiliwa.
Kocha Minziro amesema hayo katika mahojiano maalum na HabariLEO na kueleza wengi wao hawajui wanachokitafuta, wanaridhika haraka na hawajitoi kwa ajili yao, klabu na timu ya taifa.
Amesema mastraika wazawa wanapaswa kubadilika fikra na kujifunza kutoka kwa washambuliaji wageni, akiwemo Fiston Myele na Saido Ntibazokiza ambao wameonesha utofauti mkubwa tangu wasajiliwe.
“Vijana wetu wa kitanzania hawajitambui, straika anangoja kocha aje ampe mazoezi ya kufunga peke yake, akitoka pale kamaliza hajiongezi mwenyewe,” amesema na kuongeza;
“Tuna kazi kubwa sana kuweza kupata straika huyu ndio tunajivunia, tuna kazi kubwa sana, wapo mastraika lakini bado hatujasema huyu ni mfungaji haswa tuna kazi kubwa sana.
“Nawaona (washambuliaji) lakini bado hawajanivutia sana, nataka straika ambaye ananivutia, muda wote, kila wakati ana hamu ya goli,” amesisitiza.
Minziro amesema ukiweka mlinganisho wa washambuliaji wa kisasa na washambuliaji wa zamani utaona wazi kwamba washambuliaji wa zamani walikuwa na kitu cha ziada tofauti na sasa.
Ametaja baadhi ya washambuliaji wa zamani wa kuigwa nchini ni Zamoyoni Mogella, Peter Tino, Mohamed Hussein ‘Machinga’, marehemu Mohamed Chumila pamoja na Edibily Lunyamila.
“Sasa kizazi hiki sasa hivi vijana unawapa mifano kama hiyo, lakini bado hawatuelewi, unamuuliza mchezaji unaniahidi nini mechi ya leo, mchezaji yupo kimya tu, anakwambia ngoja tukapambane.
“Hakuahidi kama leo utaona naenda kufunga goli, kwa sababu hawana confidence (hawajiamini) mchezaji anaingia uwanjani anaenda kucheza tu, usiingie uwanjani kucheza tu weka dhamira yako.
“Unapaswa kuahidi mimi mechi ya leo naenda kufunga, nisipofunga leo kocha utaniambia, ndiyo maana unawaona professional (wachezaji wa kulipwa) wanafanya vizuri, kwa sababu wana dhamira yao.