ILI kuhakikisha kauli mbiu ya tunaifungua Mtwara inatekelezeka, Idara ya Uhamiaji imefungua mipaka ya Kilambo na Mkunya ili kuwezesha watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 16, 2024 na Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara, Dismas Mosha alipoongoza zoezi la upandaji miti kwenye jengo jipya la uhamiaji lililopo Manispaa ya Mtwara mikindani mkoani humo.
Amesema mipaka hiyo ilifungwa kwa muda ila kwa sasa imeshafunguliwa ili kuifungua Mtwara na watu waweze kutoka nje kutafuta fursa za biashara na za maendeleo.
Amesema wanaendelea kutoa elimu kwa umma katika ngazi zote kuanzia shule,vijiji na kata lengo ni kusisitiza usalama wa nchi.
“Tunatoa elimu kwa umma na muitikio ni mkubwa lengo ni kusisitiza usalama wa nchi mana ulinzi wa nchi yetu ni wa kila mtanzania na mtanzania mwenyewe hasa mzalendo kama katiba inavyotwambia”
“Tuna kauli mbiu yetu ya “Mjue Jirani yako” hii ni kwa ajili ya usalama wetu sisi wenyewe na hii kauli imeitikiwa na watu wote.”amesema Mosha
Aidha sababu kubwa ya kufunga mipaka hiyo ni vurugu zilizokuwa zinaendelea upande wa pili hivyo ni ngumu kumtoa mtu huku kumpeleka nchi jirani wakati kuna machafuko.
“Tuliaghirisha shughuri zetu kwasababu upande wa pili kulikuwa na vurugu, unavyomuhudumia mtu kutoka nje ya nchi unatakiwa aende kule ahudumiwe na serikali iliyopo.
“Sasa upande wa pili kulikuwa na machafuko hivyo huwezi kumtoa mtu wako aende kule kwa ajili ya biashara wakati kule hakuna mtu wa kumuhudumia, passport yetu imeandikwa kabisa Rais wa nchi anaomba mtu wangu achungwe, alindwe” amesema
Hata hivyo walowezi waliojiorodhesha hadi sasa ni 11,037 huku akiwaomba wajitokeze kujiandikisha ili waweze kuwa sehemu ya tanzania na kuacha kukaa kwa mashaka.
Sambamba na hilo amesema toka mipaka ifunguliwe kwasasa uingiaji na utokaji wa wananchi ni mkubwa Katika mpaka wa kilambo,mkunya na mtamba swala.