Mipango yaanza urithi wa riadha kwa vijana

ARUSHA: RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (SRT) Rogath Stephen amesema safari ya kuendeleza mchezo wa riadha ndio imeanza kwani shirikisho hilo litaanzisha rasmi mbio za watoto na vijana lengo ni kuwatayarisha wenye umri huo kuwa kurithi mikoba ya wanariadha wanaojiandaa kustaafu.

Stephen amesema hayo leo alfajiri alipowasili jijini Arusha akitokea Mwanza baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa SRT kuwa Rais wa Shirikisho hilo na kusema kuwa wakati umefika sasa wa kuwaanda watoto na vijana kushiriki mchezo wa riadha ili waweze kushika nafasi za akina Alphonce Simbu ,Magdalena Shauri,Jackiline Sakilu na Gabriel Geyai watakapostafu.

Amesema SRT lazima ijiandae kwa kuwaanda watoto na vijana ili waupende mchezo huo na hatimaye waweze kufanya vizuri kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kushika zile nafasi walizofanya vizuri wanariadha wenzao hivyo wale wote wanaoanzisha na walioanzisha mbio kote nchini kipaumbele ni kuanzisha mbio za watoto na vijana mara moja kwani ndio lengo la msingi la kukuza mchezo huo unapendwa kwa sasa hapa nchini.
Rais huyo amesema ajira kwa sasa ni ngumu iwe ndani ya serikali na nje ya serikali na ajira nzuri ni mchezo wa riadha hivyo aliwaasa wazazi kuwapa ushirikiano watoto na vijana kujikita katika mchezo huo kwani una pesa nyingi kwa muda mfupi na kutoa mfano Simbu aliposhinda mbio za Boston amepata fedha nyingi ambazo hata waziri akistaafu serikali hawezi kuzipata.

Rogath ambaye mwajiriwa wa jeshi la Polisi nchini na kituo chake cha kazi Polisi Kati Arusha kwa cheo cha Mrakibu Msaidizi Mwandamizi (ASP) alimshukuru sana Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Inspekta General wa Polisi, Camilius Wambura kwa kumpa baraka za kuchukua fomu za kuwania kinyang’anyanyiro hicho na hatimaye kushinda urais.



