Miradi 61 ya maji kutekelezwa Morogoro
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Morogoro katika mwaka 2022/2023 unatekeleza jumla ya miradi ya maji 61, ikiwa na thamani ya Sh bilioni 83.1.
Kaimu Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Sospeter Lutonja, amesema hayo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwenye taarifa fupi ya hali ya huduma ya maji Mkoa wa Morogoro pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji.
Waziri Aweso ameanza ziara ya wiki moja Januari 3, 2023 mkoani humo ya kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya maji.
Mhandisi Lutonja amesema kuwa miradi hiyo utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali, baadhi imekamilika na mingine inaendelea na ujenzi.
Amesema miradi 53 inatekelezwa kupitia Ruwasa na hadi kufikia Desemba 2022 jumla ya miradi 10 yenye thamani ya Sh bilioni 4.4 ilikamilika na inatoa huduma kwa wananchi.