KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdallah Shaib Kaim amesema miradi yote 17 iliyopo Halmashauri ya Bumbuli na Halmashauri ya Lushoto imetekelezwa kwa kiwango cha hali ya juu kwa kuzingatia thamani ya pesa.
Alisena kuwa utekelezaji huo mzuri umetokana na usimamizi na ufuatiliaji madhubuti wa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro.
Kaim alisema hayo wakati akiweka Jiwe la Msingi katika mradi wa maji kijiji cha Irente Yoghoi Ngulwi uliogharimu Sh milioni 578 na kufikia asilimia 90 kukamilika huku Mkandarasi Buzubona & Sons Co.ltd akiwa ameshalipwa zaidi ya Sh milioni 421.
Alisema miradi yote katika Wilaya ya Lushoto imezingatia viwango na imefuata sheria ya manunuzi na sifa zote zimwendee Mkuu wa Wilaya hiyo kwani ameona jinsi watendaji wa idara katika Halmashauri hizo wakijieleza bila ya wasiwasi.
Kiongozi huyo pia alimsifu Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Lugongo kwa jinsi anavyohakikisha maji katika Wilaya ya Lushoto yanapatikana kwa wingi kama Rais Dk Samia Suluhu Hassan anavyotaka lengo ni kutaka kumtua ndoo mama.
Alisema na kuwataka wakuu wa wilaya zingine na mameneja wa maji mkoa kuiga mfano wa viongozi hao kwani watendaji wa dhati wenye lengo la kutaka miradi yote kukamilika kwa wakati kwa faida ya watanzania.
Mradi huyo hadi sasa umekamilika kwa asilimia kubwa kama vile ujenzi wa chanzo kipya, ukarabati wa matanki mawili ya kuhifadhi maji, uchimbaji mitaro na kufikia mita 13,500,ulazaji bomba mita 13,500,uunganishaji wa bomba na fittings zake,ujenzi tanki mbili na uwekaji wa fensi katika matanki 3 ya Maji.
Vijiji Vitano huenda vikanufaika na mradi huo wa maji mkubwa katika wilaya hiyo na vijiji hivyo ni pamoja na Ngulwi, Bombo, Chumbageni, Handeni na Miegeo ambavyo vina wakazi zaidi ya 6,239 .