Miradi ya Sh bilioni 3 yacheleweshwa Arusha

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana Rushwa mkoani Arusha (TAKUKURU) imebaini ucheleweshaji wa miradi mitatu ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.8 kinyume na makubaliano katika mkataba na imewataka wakurugenzi wa halmashauri husika kuchukua hatua stahiki ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Mkuu wa taasisi hiyo mkoani Arusha, Zawadi Ngailo amezungumza hayo alipowasilisha taarifa ya robo ya mwaka ya utekelezaji wa taasisi hiyo kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana na kusema kuwa baada ya kubaini mapungufu hayo walifanya mawasiliano na wakurugenzi wa halmashauri husika pamoja na wasimamizi wa miradi hiyo wataalamu na kamati za miradi kuwahimiza kutimiza wajibu.

Ngailo alisema baada ya kukutana Takukuru walitoa ushauri kwa wataalamu na kamati za miradi kusimamia ili kuharakisha ukamirishwaji wake na baada ya hatua hiyo utekelezaji wa miradi hiyo uliendelea vizuri na mradi yote ya shule ilikamilika japo ulichelewa kwa siku siku 15.

Mkuu wa Takukuru alitaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa mpya ya sekondari SEQUIP katika kata ya Sekei jijini Arusha wenye thamani ya Sh milioni 584.2 ambao ulichelewa kukamilika kwa zaidi ya siku 30.

Mradi mwingine ni pamoja na mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana Orbomba uliopo wilayani Longido wenye thamani ya Sh bilioni 3 ambao ulichelewa kwa siku 15 na mradi wa ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya sekondari ya Mringa wilayani Arumeru wenye thamani ya Sh milioni 260 ulichela kwa siku 30.

Ngailo aliwakumbusha Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Arusha ,wataalamu na kamati za miradi kujitoa kwa kuwajibika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi yote iliyopo katika halmashauri zao kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Mkuu huyo wa Takukuru Arusha alisema katika kipindi hicho cha Oktoba na Desemba mwaka huu taasisi hiyo ilifanya uchambuzi za mifumo sita kuhusiana na utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi na kubaini utoaji wa hati milki ulicheleweshwa kwa siku 390 bila sababu za msingi.

Alisema kwa mujibu wa mwongozo wa serikali hati miliki za ardhi inapaswa kutolewa ndani ya siku 14 tu na sio vinginevyo hivyo aliziomba mamlaka husika kuhakikisha inasimamia hilo ili kuondoa kero kwa wananchi zisizo za msingi.

Ngailo alisema katika kipindi hicho Takukuru Arusha iliendelea kupokea malalamiko kwa niia mbalimbali katika kipindi hicho na jumla ilipokea malalamiko 89 kati hayo malalamiko 73 yalihusu rushwa na malalamiko 16 hayakuhusu rushwa.

Mkuu alisema katika kipindi hicho kesi 12 ziliendelea mahakamani ambapo kesi 4 ni za rushwa kubwa na kesi 8 za rushwa ndogo na zikikamilika taasisi zitatoa taarifa.

Alisema mikakati ya januari hadi marchi mwaka huu taasisi imejipanga kuendeleza programu ya Takukuru Rafiki na kushirikiana na wadau kutafuta ufumbuzi kero zote zitakazoibuliwa katika program hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inatekelzwa kwa wakati na kiwango kinachostahili.

Habari Zifananazo

Back to top button