Mitambo 8 kukabili shida ya maji Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema serikali inaendelea na maboresho ya  miundombinu ya maji ikiwemo kufunga mitambo mipya minane ya maji ili kuondoa changamoto ya upungufu wa maji katika mkoa huo.

Chalamila amesema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari.

“Hadi sasa kulikuwa na changamoto ndogo ya uchakavu wa pampu zinazopampu maji kutoka Ruvu Chini. Wizara ya Maji kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwa usimamizi wa DAWASA (Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam) zimeshaagiza pampu nane ambazo ndani ya mwezi mmoja ujao tunaamini ya kwamba pampu hizo zitakuwa zimeshafungwa ili Watanzania wote wapate huduma ya maji,” amesema.

SOMA: Dar kinara makusanyo ya maduhuli

Alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo ambao maeneo yao kuna mgao wa maji, huduma hizo za maji zitaendelea kutengemaa kuwa imara baada ya huduma hizo zitakapokuwa zimeimarishwa na mashine hizo zote zimefungwa ili kuongeza uwezo wa kusukuma maji kuwafikia wananchi.

“Yapo baadhi ya maneo ya Kimara, Kinondoni, Temeke na hapa katikati ya jiji yamelalamikiwa kuwa na upungufu wa maji. Ni kweli kwamba uzalishaji wa maji katika mkoa wetu mashine zote zikiwa safi kutoka Ruvu Juu hadi Ruvu Chini ni zaidi ya lita milioni 500.6 na matumizi yetu wananchi wa Dar es salaam huwa si chini ya lita milioni 500.43,” amesema Chalamila.

Amesema Rais Samia alijenga tangi kubwa Kinyerezi linalojengwa kwa takribani Sh bilioni 34, likiwa ni pamoja na kufunga baadhi ya pampu na katika vituo vya maji na linatarajiwa kusambaza maji kwa wananchi wa Pugu,

Ukonga, Kimbamba, Segerea na Kinyerezi. Ameongeza: “Matangi hayo yameshakamilika, kilichopo sasa ni kuanza kubadilisha mfumo wa mabomba yanayotumika kusafirisha maji kwenda kwa wananchi. Ninaamini baada ya kukamilisha zoezi hilo, wananchi wote watapata maji katika maeneo yote yenye changamoto.”

Wakati huohuo, amesema serikali inaendelea na maboresho ya sekta ya nishati na miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kuboresha uchumi, maisha na ustawi wa Watanzania.

Chalamila amesema mahitaji ya umeme kwa Mkoa wa Dar es Salaam si chini ya megawati 650 na mkoa huo una vituo vinavyofanya uzalishaji wa umeme wa gesi si chini ya sita, ikiwemo cha Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II, Ubungo III na Tegeta.

Amesema vituo vyote vina uwezo wa kuzalisha megawati 952 na mkoa huo unatumia si chini ya megawati 650 kwa wananchi walioingiziwa umeme milioni 1,300,000 pamoja na kupeleka umeme kwenye viwanda.

“Miradi ya umeme inayoendelea Dar es Salaam kwa sasa ina thamani ya Shilingi trilioni 1.3 ambazo zinatumika kubadilisha nguzo za miti kuweka za zege, kuimarisha vituo vidogo vya uzalishaji umeme vya Mabibo, Mbagala na sehemu nyinginezo. “Pia, kubadilisha nyaya kwa kuweka zenye uwezo mkubwa na kununua mitambo mingine, ikiwemo transfoma kwa ajili ya kuongeza kasi ya uzalishaji na uzambazaji wa umeme,” amesema Chalamila.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatambua umuhimu wa umeme katika mkoa huo, kwa sababu kuwepo kwa umeme wa uhakika kutaongeza uzalishaji katika jamii.

Pia, Chalamila amesema serikali inaendelea na ujenzi wa barabara na madaraja makubwa ili kuondoa adha ya kufungwa kwa barabara kipindi cha mvua kubwa.

“Zimeshatolewa Shilingi bilioni 67 zilizoanza kujenga daraja lenye meta 390 kutoka upande wa Magomeni kwenda Fire ambalo kutoka chini kwenda juu lina urefu meta 10, kwa maana hiyo maji kufika kwenye barabara itakuwa ni historia na limeshaanza kujengwa na litatumia miaka miwili hadi kukamilika,” alisema.

Alitaja madaraja mengine yanayojengwa kuwa ni Daraja la Kigogo la upana wa meta 50 linalojengwa kwa Sh bilioni 17, Daraja la Mkwajuni la thamani ya Sh bilioni 11.6, Daraja la Mtongani la thamani ya Sh bilioni 24.6 na Daraja la Nguvu linalojengwa kwa Sh bilioni 92.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button