TUME ya Maendeleo ya Ushirika Nchini (TCDC), imeazimia kuanza kutumia mizani ya kidigitali katika ununuzi wa zao la pamba, ili kuondoa udanganyifu wa wanunuzi kuminya haki ya wakulima katika vipimo.
Ofisa Mrajis wa TCDC, Dk Benson Ndiege ameeleza hayo leo Desemba 28, 2022 katika mahojiano maalum na HabariLeo, juu ya mikakati ya kuhakikisha kilimo cha pamba kinawanufaisha wakulima.
Dk Ndiege amesema mizani ya kidigitali itatolewa kwa Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS), ambao ndio wasimamizi wa masoko, ili mkulima aweze kupata kipimo na malipo sahihi.
“Kwa maana kwamba ile mizani ya kusogeza kwa mikono kuna mkulima anatoka kijijini hajui kusoma ile mizani, na akiwa pale yeye anambiwa ni kilo 50 kumbe ni kilo 70.
“Pamoja na kwamba bei inaweza kuwa rafiki bado unaweza kukuta mkulima amepunjwa kwenye uzito, kwa hiyo tutagawa mizani hiyo kwenye vyama vyote vya ushirika,” amesema.
Amesema mizani ya kidigitali itamuwezesha mkulima kung’amua uzito wa mzigo wake kwa uwazi na kupatiwa risiti yenye vielelezo vyote, ikiwemo uzito wa pamba na thamani halisi.