Mkakati wawekwa kuongeza thamani madini

SERIKALI imeweka mkakati  kuhakikisha madini yote yanaongezwa thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika hafla ya kuadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwa Kampuni ya PULA Group.

“Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi wasaidizi wake kuhakikisha tunasimamia uongezaji thamani wa rasilimali madini ili yanufaishe Watanzania wengi zaidi,” amesema Mavunde na kuongeza:

” Ndiyo maana tunasimama kifua mbele kutekeleza maagizo hayo ya Serikali kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” amesema na kueleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona madini yote yanasafirishwa yakiwa yameongezwa thamani.

“Na ndiyo maana tumeweka mkakati ambao pamoja na kuvutia uwekezaji, tumeweka sharti la uwekezaji huo uendane samamba na uongezaji thamani wa madini yatakayochimbwa”, amesisitiza Mavunde.

Ametoa rai kwa wawekezaji kuchamgamkia fursa ya uwekezaji, kwani Tanzania imejaaliwa madini ya aina nyingi, mazingira mazuri ya uwekezaji na miundombinu ya kisasa ambayo yanarahisisha uwekezaji wa aina yeyote katika sekta ya madini.

Wakati huo huo Mavunde amesema Tanzania ipo tayari kupokea wawekezaji katika madini mkakati na muhimu na tayari kuna utaratibu maalum ambao utawezesha kuyaongeza thamani hapa nchini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi.

“Ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita kwenye sekta ya madini ambapo, tunahitaji betri za kufungwa kwenye magari ya umeme zitengenezwe hapa nchini Tanzania na kupelekwa kufungwa kwenye magari moja kwa moja popote pale duniani”, alibainisha Mavunde

Awali, akitoa salamu zake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania,  Dk Michael Anthony Battle alieleza kuwa dunia kwa sasa imeweka kipaumbele katika nishati safi, ambayo inatokana na madini muhimu na mkakati, na kutoa wito kwa Tanzania kuwalazimisha na kuwaomba wawekezaji wote watakaofika kwenye sekta ya madini sharti waongeze thamani hapa hapa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya PULA, Balozi Charles Stith alibainisha kwamba hakujiuliza mara mbili kuleta uwekezaji nchini Tanzania kutokana na kubarikiwa uongozi thabiti na imara unaovutia na kulinda maslahi ya wawekezaji na kuongeza kuwa PULA inakwenda kuifanyaTanzania kama kitovu katika uwekezaji inaokwenda kupanua katika nchi zingine jirani kama Malawi.

Habari Zifananazo

Back to top button