Mkandarasi atakiwa kuongeza kasi mradi wa maji

NAIBU Waziri wa Maji, Kundo Mathew amemtaka mkandarasi anayejenga mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kupeleka Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu ,mkoani Mtwara kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 38.1.

Ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka huu kutarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu. Mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 52 tu.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi, Waziri Kondo amesema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi licha ya kuwa mkandarasi huyo ameshalipwa sehemu ya gharama ya mradi Sh bilioni 20.

Advertisement

‘”Mradi huu mpaka sasa ulitakiwa ukamiliki miezi miwili ijayo lakini kwa kasi asilimia na ‘progress’ ya mradi akiangalia na muda uliobaki ninapata mashaka sana kuwa mradi utakamilika kwa wakati,” amesema.

Amemtaka mkandarasi huyo wakishirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Masasi, Nachingwea (MANAWASA) kuongeza watu ili kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi kwa wakati.

Mradi huo unajengwa na serikali kushirikiana na serikali ya India kupitia Mkandarasi wa M/S AFCONS Infrastructure Limited pamoja na Mtaalamu Mshauri WAPCOS Limited.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Christopher Magala amesema upatikanaji wa maji Wilaya ya Nanyumbu ni asilimia 37 tu huku alisema kukamilika kwa mradi utaongeza uzalishaji mpaka kufikia asilimia 85 na kuendelea.