WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum, George Mkuchika amezipongeza taasisi za dini nchini kwa kujitoa kushiriki katika kutoa huduma za kijamii kwa Watanzania bila kujali imani za kidini.
Mkuchika ametoa pongezi hizo katika kilele cha Jubilee ya miaka 75 ya Shirika la Masista wa Chama Cha Mariam Mtakatifu (CMM) wa kanisa la Angalikana nchini Dayosisi ya Masasi.
“Kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, napenda kuwapongeza sana taasisi za dini nchini kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kutoa huduma za jamii, bila kujali imani za kidini,” amesema.
Mkuchika amesema serikali pia imekuwa ikinufaika na huduma za dini, akitolea mfano wa watumishi wa umma ambao wengi wao walisoma katika shule ambazo zinaanzishwa na kuendeshwa na taasisi za dini nchini.
Ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini, katika kustawisha maisha ya Watanzania.