Mkurugenzi aongoza zoezi udhibiti magonjwa ya mifugo

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mutallah Mbillu ameongoza zoezi muhimu la kuogesha mifugo katika eneo la Lata  Kata ya Oloipiri, linalolenga kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa ndigana baridi unaowaathiri mifugo mbalimbali wakiwemo ng’ombe.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni mkakati wa  kuimarisha juhudi za ufugaji ambapo, Mbillu ametoa msaada wa lita 12 za dawa ya kuogesha, ambayo itawawezesha wananchi kuogesha mifugo yao bure.

Advertisement

Akizungumza wakati zoezi hilo, Mbillu amewasisitiza wafugaji kuogesha mifugo yao kila baada ya siku saba badala ya desturi ya kuogesha kila mwisho wa mwezi, ili kuhakikisha kinga madhubuti dhidi ya ndigana baridi.

Ameeleza kuwa afya bora ya mifugo ni muhimu kwa ustawi wa kiuchumi wa halmashauri hiyo, kwani wafugaji ni nguzo kuu ya mapato ya halmashauri.

Huku Ofisa  Kilimo, Mifugo, na Uvuvi wa wilaya hiyo,Chobby Chubwa, amesema katika kuhimiza wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, alibainisha kuwa ugonjwa wa ndigana baridi unaweza kudhibitiwa kwa njia ya kuogesha mara kwa mara.

Alieleza kuwa asilimia 70 ya magonjwa ya mifugo hutokana na kupe, hivyo kuogesha mifugo ni hatua muhimu katika kuboresha afya ya mifugo.

Huku mfugaji ,Ramatho Saringe, kutoka kijiji cha Oloipiri, ameishukuru serikali na halmashauri kwa kuanzisha na kusimamia zoezi hilo kwani  hatua hiyo itasaidia kudhibiti ugonjwa wa ndigana baridi ambao umekuwa changamoto kubwa kwa mifugo yao.