MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ameridhishwa na maandalizi na utayari wa wanafunzi wa kidato cha nne wanaoendelea na mitihani ya taifa.
Wanafunzi wa kidato cha nne walianza kufanya mtihani wa taifa kuanzia jana. Mafuru alisema kutokana na utayari walioonesha wanafunzi, halmashauri inategemea matokeo mazuri.
Mafuru aliyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kufanya ukaguzi mwishoni mwa wiki kabla ya wanafunzi hao kuanza mtihani wa taifa.
“Nimetembelea shule ya sekondari za jiji hili kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mwisho kuangalia kama maandalizi yote yako sawa, nimeridhishwa na maandalizi na utayari wa wanafunzi kwa ajili ya mitihani hii,” alisema.
Alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina imani kuwa wanafunzi wake watafanya vizuri kwenye mitihani yao kutokana na kuendesha programu maalumu ya kuwanoa ili kujiandaa na mtihani huo.
Mafuru alisema taarifa ya awali inaeleza wanafunzi hao walikuwa na uwezo wa chini lakini kutokana na kufanyika kwa programu hiyo maalumu, uwezo wao umeimarika na kuwa mzuri.
“Nimejionea, nimeenda nimekutana na wanafunzi wana ari kubwa ya ufaulu.
Nimshukuru Ofisa Elimu Sekondari, Upendo Rweyemamu ambaye ndiye aliyeleta hii programu kwa Jiji la Dodoma na kuwasilishwa katika Baraza la Madiwani ambao waliliridhia.”
“Tumeona kujiamini kwa watoto, ogopa mtoto anayekwambia lete mtihani hata leo, maana yake wapo tayari. Matarajio ya Jiji ni matokeo bora zaidi ya msimu uliopita,” alisema.
Kwa upande wake, Rweyemamu alisema: “Tuna jumla ya watahiniwa 6,647 na kati yao, wavulana ni 3,019 na wasichana ni 3,628.
Tulianza kuwaandaa wanafunzi hawa muda mrefu. Tumekuwa na programu mbalimbali kama za shule kwa shule na za ndani ya wilaya.”
Alisema programu maalumu kwa wanafunzi walioonekana kuwa na ufaulu hafifu wamefundishwa kupitia programu maalumu ili waweze kuongeza ufaulu wao.
“Tuliwatengenezea mazingira ya kuwaweka pamoja na kikosi kazi cha walimu 56 wamekuwa nao kwa zaidi ya miezi miwili.”
“Hivi karibuni tuliwapa mtihani wa jaribio na wanafunzi wengi walipata daraja A na B katika masomo yao. Wanafunzi hawa tumewaandaa vizuri na hata kisaikolojia wapo tayari kukabiliana na mtihani.”
Aliongeza: “Unapowekeza mahali unategemea kupata mabadiliko ama mavuno mazuri. Mwaka jana tulikuwa na daraja la I (652) kati ya wanafunzi 55,326. II (524), III (1,012), IV (2,735) na O (403). Tulipata ufaulu wa asilimia 93 na GPA ya 3.1. Kwa mikakati tuliyoweka na programu tunazofanya tutapunguza sana daraja 0. Lakini daraja la I-III litaongezeka sana.”
Ofisa elimu huyo alilishukuru Baraza la Madiwani kwa kuwa msaada kwa idara yake.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina vituo 54 vinavyofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu