Mkutano Bunge jipya kuanza leo

MKUTANO wa kwanza kwa Bunge la 13 la Tanzania unaanza leo jijini Dodoma ambao pamoja na masuala mengine, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua bunge hilo jipya.

Taarifa ya Katibu wa Bunge, Baraka Leonard imeeleza shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kusomwa Tangazo la Rais la kuitisha Bunge na kufanya uchaguzi wa Spika wa Bunge.

Spika wa Bunge la 12 alikuwa Dk Tulia Ackson aliyechukua majukumu hayo baada ya Job Ndugai kujiuzulu. Shughuli nyingine katika mkutano huo ni kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu na uchaguzi wa Naibu Spika.

Leonard alieleza kwamba katika mkutano huo pia utafanyika ufunguzi wa bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bunge la 13 linatarajiwa kuwa na wabunge 272 wa majimbo yakiwemo 222 ya Tanzania Bara na 50 ya Zanzibar kukiwa na ongezeko la majimbo manane Tanzania Bara.

Bunge hilo pia litakuwa na wabunge 115 wa Viti Maalumu wakiwemo 113 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wawili wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).

Bunge la 12 lilimaliza shughuli zake Juni 27 mwaka huu na lilivunjwa Agosti 3, mwaka huu. Kwa kuzingatia Katiba, bunge hilo lilikuwa na wabunge 393 wakiwemo 264 wa majimbo.

Majimbo 214 kati ya hayo yalikuwa ya Tanzania Bara na 50 ya Zanzibar. Lilikuwa na wabunge 113 wa Viti Maalumu, 10 wa kuteuliwa na Rais wakiwemo wanawake watano, watano kutoka Baraza la Wawakilishi wakiwemo wanawake wawili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika bunge hilo, kwa upande wa wabunge wa majimbo, CCM ilikuwa na wabunge 255, Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa na watatu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilikuwa na mmoja na Chama cha ACT Wazalendo kilikuwa na wabunge wanne.

Pia, katika Bunge la 12, CCM kulikuwa na wabunge 94 wa viti haalumu na kufanya jumla kuwa na wabunge 364. Chadema walikuwa na wabunge 19 wa viti maalumu na kuwa na wabunge 20.

Bunge la 12 lilikuwa na wabunge 148 wanawake wakiwemo 28 wa majimbo. CCM ilikuwa na wabunge 25 wa majimbo, CUF wawili na Chadema mmoja.

Kwa mgawanyo wa wabunge wa pande mbili za Muungano, wabunge 312 walitoka Tanzania Bara na 79 wa Zanzibar.

Aina za wabunge Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge, inataja aina sita ya wabunge kuwa ni pamoja na waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi na wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake.

Wengine ni wabunge wanawake wa idadi inayoongezeka kuanzia asilimia 20 ya wabunge watakaochaguliwa na vyama vya siasa vinavyowakilishwa bungeni kwa mujibu wa Ibara ya 78 na kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama hivyo.

Wabunge wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wabunge wasiozidi 10 walioteuliwa na Rais na Spika wa Bunge iwapo hatakuwa amechaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge.

Matarajio Wadau wa siasa wamesema wanatarajia kuona Bunge la 13 likizingatia maslahi ya taifa na lisiloegemea itikadi za vyama.

Mbunge mteule wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia ACT Wazalendo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema anatamani Bunge la 13 lisisitize uwazi na uwajibikaji.

“Natamani tusimamie maslahi ya taifa na si vyama vyetu wala sisi binafsi kwa sababu Watanzania wanatutazama kwa matumaini makubwa. Nitafarijika kuona tunashikamana na kuwa wamoja bila kujali rangi za vyama vyetu katika masuala ya kitaifa,” alisema Shaibu.

Alishauri Bunge la 13 lifanyie kazi suala la ajira kwa vijana. “Natarajia bunge hili lipiganie suala la ajira kwa vijana kwa kuhamasisha uchumi jumuishi utakaosaidia kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wetu walioko mtaani,” alisema Shaibu.

Mbunge huyo mteule alishauri yafanyike maridhiano kulinda amani, utulivu na mshikamano ili kulinda heshima ya nchi sanjari na kuandaa katiba mpya itakayofanyia kazi changamoto zilizolalamikiwa na wananchi.

Mhadhiri katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na mchambuzi wa siasa, Zacharia Swedi ameshauri Bunge la 13 lifanyie kazi suala la uchumi ukiwemo wa mtu mmoja mmoja. Swedi alisisitiza bunge lijadili siasa kwa kutazama yaliyopita ili yasijirudie, pia ishughulikie kero za Muungano.

“Tunatarajia watu wengi wakijipambanua kwa kuwa tofauti na wale tuliowazoea. Hivyo, tunadhani kutakuwa na changamoto kidogo zitakazoletwa na hawa wapya, lakini hata wale wa zamani ikiwa kuna hoja zinazoshawishi na zenye mrengo wa kuleta maendeleo endelevu,” alisema.

Mhadhiri katika Shule Kuu ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Omary Mbura alisema anatarajia bunge hilo litasaidia Watanzania kutoka kwenye uchumi wa kati na kusogea kwenye uchumi wa juu.

“Bunge hili lina mchanganyiko japo wengi ni CCM, hiyo ni ishara kwamba tutapata mawazo mchanganyiko yatakayosaidia kuchochea maendeleo,” alisema Profesa Mbura.

Alitoa mwito kwa wabunge watumie nafasi zao vizuri ili kuifikia Tanzania yenye uchumi unaotakiwa kwa kuwa miaka mitano ni muda mfupi.

“Tumeona hoja nyingi zikitolewa bila taarifa sahihi, mwisho wa siku zinapoteza muda bungeni na wakati mwingine kusababisha wengine kuitwa kwenye kamati za maadili. Hatutamani hili litokee tena, muda utumike kwa ufanisi ili kukamilisha jukumu walilopewa na wananchi,”alisema Profesa Mbura.

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo alisema anatarajia liwe bunge lisiloegemea misimamo ya vyama.

“Lazima wajue kuwa bunge ni msimamizi mkuu wa serikali kwa mujibu wa katiba na si chombo cha kisiasa,” alisema Doyo.

Aliongeza: “Maamuzi mengi yatategemea uzalendo wa wabunge kwa yale yatakayokuwa na faida kwa wananchi. Nashauri bunge liwe la wananchi na si la chama cha siasa”.

Doyo alisema suala la maji, umeme na afya ni mambo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ili kuleta manufaa kwa taifa, bila kusahau ahadi aliyoitoa Rais Samia wakati wa kampeni.

Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru aliwashauri wabunge wawe wazalendo na wazungumze ukweli.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button